Wednesday, 29 February 2012

KUTOKA GAZETI LA MWANANCHI: BALOZI MAHALU AMLIPUA JK MAHAKAMANI

Anika alivyoshiriki katika mchakato kipindi akiwa waziri mambo ya nje, Asema alikutana na mama mwenye nyumba na kuagiza alipwe dola milioni moja haraka, Akampa ofa kuja mbuga ya ngorongoro

Na Tausi Ally

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, 
Profesa Costa Mahalu

ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alifahamu kuwepo kwa rasimu mbili za mikataba ya ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania, Italia.

Profesa Mahalu alisema hayo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Ilvin Mgeta wakati akitoa utetezi wake dhidi ya kesi inayomkabili ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 pamoja na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin.

Akiongozwa na wakili wake, Mabere Marando, Profesa Mahalu aliitambua barua ya Februari 20, 2002 ambayo ilikuwa ikieleza kuwa matayarisho yote ya ununuzi wa jengo la ubalozi huko Italia yamekamilika ikiwa ni pamoja na rasimu mbili za mikataba.

Mahalu alidai kuwa katika mchakato wa ununuzi wa jengo hilo wakati yeye akiwa Balozi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kulikuwa na rasimu mbili za mikataba na kwamba aliwahi kuwasiliana na wizara hiyo juu ya mikataba hiyo.

Alidai kuwa Desemba 2001, Kikwete wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alikwenda Rome, Italia kwenye Mkutano wa SADC na alipokuwa huko, ubalozi ulifanya mpango atembelee jengo hilo lililopendekezwa kununuliwa kwa ajili ya ofisi ya ubalozi.

“Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia ilifanya mipango yote kwa kumpa utaratibu na usalama Kikwete ambapo alikwenda kutembelea jengo hilo na kukutana na mama mwenye jengo,” alidai Profesa Mahalu.
Alidai kuwa kabla ya mazungumzo na mwenye nyumba, mtoto wa mama huyo, Alberto alimtembeza Kikwete kwenye jengo hilo ndani na nje na baadaye mazungumzo hayo yaliendelea.

Balozi Mahalu alisema baadaye mazungumzo kati ya Kikwete na mama huyo yaliendelea na Alberto alikuwa akitafsiri, kwa sababu mama yake hakufahamu lugha ya Kiingereza.

Profesa Mahalu alidai kuwa katika mazungumzo hayo, Kikwete alimwuliza mama huyo: “Hivi ni kwa nini kunakuwa na mikataba miwili?” na mama huyo alimjibu kuwa hiyo ni kawaida kwa Italia ukitaka kununua jengo kwa bei nafuu.

Profesa Mahalu aliendelea kudai kuwa baada ya kupewa jibu hilo, Kikwete hakuzungumza tena zaidi ya kucheka na kwamba mwenye jengo alimkumbusha kuhusu malipo ya awali ya dola milioni moja za Marekani ambapo aliafiki na kuahidi kuwa zingelipwa kabla ya mwisho wa mwaka 2001.
Profesa Mahalu alidai pia kwamba Kikwete alimweleza mama huyo kuwa atalishughulikia suala hilo baada ya kurejea Dar es Salaam na kumshukuru kwa kuwauzia jengo zuri.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Profesa Mahalu alidai kuwa baada ya Kikwete kusema maneno hayo, alimgeukia na kumwambia: “Costa ni vizuri tupate hela tumlipe huyu mama watu wengine wasije wakachukua hili jengo.”

Profesa Mahalu alidai kuwa baada ya Kikwete kumshukuru mama huyo kwa ukarimu wake, alimkaribisha Tanzania awe mgeni wa Wizara ya Mambo ya Nje yeye na mumewe na kwamba watampeleka Ngorongoro.

“Tulipokuwa njiani tukirudi hotelini alipofikia Kikwete akiwa kwenye gari alimpigia simu Kibero akimuagiza afanye utaratibu wa kulipa Dola milioni moja kama malipo ya awali ya jengo hilo,” alidai Profesa Mahalu.

Alidai kuwa baadaye alimwagiza (Profesa Mahalu) aje Dar es Salaam kufuatilia mpango huo wa malipo ya awali ya ununuzi wa jengo hilo.

Awali, Profesa Mahalu akiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa alidai kuwa anaitambua ripoti ya uthamini wa jengo hilo la ubalozi nchini Italia uliofanywa na Kimweri kutoka Wizara ya Ujenzi aliyekwenda Rome Julai 15 hadi 26, 2001 kwamba jengo lilikuwa na gharama ya Sh6 bilioni.

Pia alizitambua ripoti za uthamini wa jengo hilo ambazo ni ile ya mama mwenye nyumba ambayo ilionyesha kuwa jengo hilo lilikuwa na thamani Sh5.500 bilioni na ripoti ya uthamini iliyofanywa na Serikali ya Italia iliyoonyesha kuwa jengo lilikuwa na thamani ya Sh11.117 bilioni.