Waandishi Wetu
SIKU
chache baada ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless
Lema kuwataja mawaziri wawili na mmoja aliyewahi kuwa Waziri Mkuu
kwamba, wameomba kujiunga na chama hicho cha upinzani, wawili kati yao
wamejitokeza na kuzungumzia madai hayo.
Waziri
Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta ambao walitajwa na Lema, jana kwa nyakati
tofauti walibeza madai hayo.
Jumamosi
iliyopita, Lema akiwa wilayani Sengerema, Mwanza alisema mawaziri
watatu, akiwamo mmoja aliyewahi kuwa waziri mkuu wameiomba kujiunga na
Chadema lakini mmoja kati yao amekataliwa na wengine mchakato wa
kuyakubali maombi yao unaendelea.
Katika
mkutano huo, Lema aliwataja mawaziri hao kwa jina moja kuwa ni Sitta,
Lowassa na waziri mwingine ambaye tunahifadhi jina lake kwa kuwa
hakupatikana jana kuzungumzia madai hayo.
Msimamo wa Sitta
Sitta
alipuuza madai hayo akiyaita ya kitoto na kueleza kuwa kwa hadhi yake,
hawezi kuomba kujiunga Chadema na kusubiri majibu kama amekubaliwa au
la.
“Yaani mimi niombe kwenda Chadema halafu
nikae kabisa huku nikisubiri wanijibu! Huo ni upuuzi na jambo hili
haliwezekani na si kweli hata kidogo. Kama Lema kasema hivyo, basi huo
ni utoto na siasa za kihuni,” alisema Sitta.
Sitta
huku akicheka aliongeza: “Sasa nimeomba kwa nani na kwa njia ipi ya
mdomo au maandishi? Mimi siyo gamba. Ni mtu mwadilifu siwezi kujiunga
katika utaratibu wa kuchukua magamba ndani ya CCM.”
“Wao
Chadema wanachukua tu kila mtu. Wakienda kwenye mikutano pia wanachukua
tu watu, sasa hivi wanachukua magamba CCM. Mimi nawatakia kila heri
katika kuchukua magamba CCM.”
Sitta alisema
yeye ni mwanasiasa makini na mwadilifu hawezi kukaa chungu kimoja na
magamba... Wanalofanya kuchukua magamba ya CCM ni faraja hata kwa Katibu
Mkuu Wilson Mukama.”
Mbunge huyo wa Urambo
Mashariki, alisema kuchukua magamba CCM ni sawa na mtu ambaye anakwenda
kwa jirani ambaye nyumba yake imezungukwa na takataka kisha akamsaidia
kuzisomba kwenda kuzitupa... Hapo si lazima ufurahie bwana?
Alisema
kama angekuwa anajiunga na Chadema wangemkumbatia akisema: “Kama
wanakwenda watu wadogo wanaandaa sherehe kubwa, nikienda mimi...?
Majibu ya Lowassa
Jana,
Lowassa naye alipuuza madai hayo ya Lema akisema hajawahi kuomba
kujiunga na Chadema huku akisisitiza: “Kama ingekuwa hivyo isingekuwa
siri. Ningetangaza uamuzi wangu kupitia vyombo vya habari.”
Lowassa
alitoa kauli hiyo baada ya gazeti hili kumtaka azungumzie madai ya Lema
kwamba aliomba kujiunga na chama hicho cha upinzani lakini akakataliwa.
“Kama
ningeomba kuingia Chadema ningetangaza kwenye vyombo vya habari.
Sijasikia hayo na sitaki kusema chochote zaidi,” alisema Lowassa na
kisha kukata simu.
Slaa amshangaa Lema
Alipoulizwa kuhusu madai hayo ya Lema, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema hawezi kuzungumzia kauli ya mtu.
“Tabia
yangu huwa sipendi kuzungumzia kauli aliyoitoa mtu hivyo alichokisema
Lema mtafuteni yeye mwenyewe afafanue kwani atakuwa anajua alichokisema
kina maana gani,” alisema Dk Slaa.
Dk Slaa
alisema: “Badala ya kukaa na kuzungumzia kauli ya mtu, kinachotakiwa ni
kujadili jinsi gani ya kuhakikisha tunapunguza ugumu wa maisha kwa
mwananchi wa hali ya chini.”
“Tuache kuzungumza
kauli za watu hapa sasa kinachotakiwa kila mmoja wetu kwa nafasi yake
atizame ni jinsi gani atahakikisha anamkomboa mwananchi kwa kupunguza
gharama za maisha.”
Lema ang’ang’ana
Hata
hivyo, jana alipotakiwa kufafanua kauli yake baada ya kuelezwa kwamba
aliowataja wabeza madai yake, Lema aliendelea kusisitiza kwamba
alichosema ni cha kweli.
“Wanakataa tu kisiasa,
lakini nilichosema ni cha kweli na (kesho), leo katika mkutano wangu wa
Singida, pamoja na kuwarudia hawa niliowataja nitawataja wengine pamoja
na wabunge wa CCM ambao wapo tayari kujiunga na Chadema.”
Katika
madai yake ya kwanza aliyotoa Jumamosi iliyopita katika mkutano
uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnadani, Lema alisema viongozi wenye
uchungu na taifa hili ndani ya CCM na ambao wamekuwa hawafurahishwi na
ubadhirifu wa mali za nchi, wamekuwa wakifanya mazungumzo kutaka
kujiunga na Chadema.
Alisema kwa vile chama
chake kimejiandaa kuingia madarakani kwa kutumia nguvu ya umma, ndiyo
maana mawaziri wa Serikali ya CCM wameomba kujiunga nacho ili kusaidiana
kwa pamoja kwenda kuingia madarakani mwaka 2015.
“Lakini,
Lowassa tumemkataa. Tunataka wachapa kazi na wenye mioyo ya kweli
katika mapambano ya kupigania haki na kuondoa dhuluma kwa Watanzania,”
alisema Lema.
Lema alidai kuwa mawaziri hao
(waliokubaliwa) wanasubiri muda muafaka ufike waweze kutangaza rasmi
kujiunga na chama hicho, kutokana na kile kilichodaiwa kuchoshwa na
mwenendo mzima wa uongozi na utendaji serikalini na ndani ya CCM,
hususan suala la kuwalinda watu wanaotuhumiwa kwa ubadhilifu.
Frederick Katulanda, Mwanza; Fidelis Butahe na Ibrahim Yamola, Dar
No comments:
Post a Comment