NI
NINI hasa kinachomsibu Dk. Harrison Mwakyembe? Je, kuna ukweli kuhusu
"kulishwa sumu" kama ilivyonenwa na Sitta? Bado utata utata unaghubika
suala hili, hivi, ni serikali haitaki kuzungumzia suala hili? Ni wazi
kabisa kwamba uchunguzi wa madaktari upo wazi kabisa, sasa utata
unapokuja kwanini kutupiana mpira juu ya nani azungumzie suala hilo
ndicho kitu pekee kinaleta wasiwasi mkubwa kwamba kuna siri nzito juu ya
afya yake.
Itakumbukwa
kwamba, Desemba 10 mwaka jana, Dk Mwakyembe akiwa na hali mbaya
alipelekwa katika Hospitali ya Appolo, nchini India kwa matibabu baada
ya kuugua maradhi yaliyosababisha ngozi yake kuharibika. Tangu arejee
mwanzoni mwa mwezi uliopita alikuwa hajaonekana hadharani, mbali na
kutoa tamko kwamba afya yake ilikuwa inaendelea vizuri.
Hata
hivyo, muda wote huo aliokuwa nchini India na baada ya kurudi nchini,
mazungumzo ya watu maofisini, nyumbani, mitaani na vijiweni yalitawaliwa
na utata wa suala la afya ya Dk Mwakyembe, huku uvumi, tetesi na
minong’ono kwamba maradhi yake yalisababishwa na hujuma za kisiasa
vikitawala hisia za wananchi. Hisia hizo zilikuzwa na kauli ya mmoja wa
washirika wake kisiasa, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samwel Sitta ambaye alimtembelea hospitalini nchini India na baadaye
kukiambia kituo kimoja cha televisheni hapa nchini kwamba Dk Mwakyembe
alikuwa amelishwa sumu kutokana na msimamo wake dhidi ya mafisadi.
Akizungumza
huku akionyesha kujiamini, Waziri Sitta alisema muda wote aliokaa na
naibu waziri huyo katika Hospitali ya Appolo alipata ushahidi wa kutosha
kwamba maradhi yake ya kuharibika kwa ngozi ya mwili wake
yalisababishwa na kulishwa sumu, huku ushuhuda wake ukiacha kitendawili
cha nani hasa waliohusika na uhalifu huo pasipo kuteguliwa. Hata hivyo,
kauli hiyo ya Waziri Sitta iliwaudhi viongozi wengi serikalini na katika
chama chake cha CCM ambao walimtaka athibitishe tuhuma kwamba hujuma
kwa Dk Mwakyembe ilikuwa ni kazi ya mafisadi.
Lakini
jambo la kushangaza ni kwamba muda wote huo Serikali ilikataa kutoa
tamko siyo tu kuhusu maradhi yanayomsumbua kiongozi huyo, bali pia kama
ilikuwa imefanya upelelezi kuhusu kuwapo au kutokuwapo watuhumiwa wowote
ambao walikuwa wanahusishwa na hujuma hiyo. Wananchi walishangazwa na
hatua ya Serikali kuendelea kukaa kimya na kupiga danadana suala hilo,
huku viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Afya wakitupiana
mpira.
Tunashangazwa
na ukimya huu wa Serikali hata baada ya kupata ripoti ya madaktari wa
Hospitali ya Appolo ambao walimtibu Dk Mwakyembe. Haki ya wananchi kujua
maradhi yanayomsibu inapewa uzito na ukweli kwamba yeye siyo tu mbunge
wa kuchaguliwa na wananchi, bali pia ni naibu waziri katika Serikali
ya Awamu ya Nne. Tukitilia maanani kwamba gharama kubwa za matibabu yake
zimelipwa kwa kodi za wananchi, ndipo tunaposhangaa kwa nini Serikali
haioni uhalali wa wananchi kujua hali ya afya za viongozi wao kwa madai
kwamba masuala ya afya zao ni masuala binafsi.
Alipojitokeza
hadharani mwishoni mwa wiki akiwa na washirika wake wa kisiasa katika
uzinduzi wa programu ya moja ya madhehebu ya Kikristo jijini Dar es
Salaam, Dk Mwakyembe aliwaeleza waumini jinsi maradhi yake ilikuwa kazi
ya mafisadi ambao walimsababishia mateso makubwa na kuahidi kuzungumzia
suala hilo kwa undani katika siku za usoni, huku Waziri Samwel Sitta
akisimama na kuwaeleza waumini kwamba Dk Mwakyembe alilishwa sumu.
Sisi tunadhani ukimya huu wa Serikali umeiletea aibu kubwa na kuibua hisia kwamba, pengine nayo ni sehemu ya tatizo. Vinginevyo haiingii akilini jinsi Serikali siyo tu inavyoweza kupata ujasiri wa kuficha ripoti iliyotolewa na Hospitali ya Appolo, bali pia kushindwa angalao kutoa tamko kama Dk Mwakyembe alilishwa sumu au la.
Kwa
kuwa Dk Mwakyembe anajua fika nini kilichomo katika ripoti iliyotolewa
na hospitali hiyo ya nchini India, tunamshauri ajitokeze hadharani
awaeleze wananchi ukweli kwa lengo la kumaliza uvumi, tetesi na
minong’ono kuhusu maradhi yanayomsibu.
No comments:
Post a Comment