Serikali yaomba madaktari nje ya
nchi
• Bilioni 200 zatengwa
kuwalipa
na Martin Malera, Dodoma
SERIKALI imeamua kuagiza madaktari kutoka nchi za nje
watakaochukua nafasi ya wale wa hapa nchini ambao wamegoma kuanzia mwishoni mwa
wiki iliyopita.
Habari kutoka katika moja ya vyanzo vya kuaminika zimesema
kuwa uamuzi huo wa serikali ulipitishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri
kilichokutana mjini Dodoma juzi chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilidai kuwa Rais Kikwete
alikerwa na tabia ya madaktari kupingana na serikali licha ya juhudi zote
zilizofanywa kuboresha maslahi yao.
Kwa mujibu wa habari hizo, kiasi cha sh bilioni 200
kimetengwa kwa ajili ya kuwaleta na kuwagharimia madaktari hao wa nje na
pia baraza limepitisha azimio la kuzungumza na hospitali za jeshi kama
Lugalo na zingine ndogo kubeba jukumu hilo kwa sasa pamoja kuagiza madaktari
wastaafu wote warejee kazini katika kipindi hiki cha mgomo.
Habari zimedai kuwa madaktari hao wanasadikiwa watatoka
katika nchi rafiki, zikiwemo India, China, Cuba na Afrika Kusini, na kwamba
wataziba kikamilifu pengo la wale wa hapa nchini ambao wamegoma.
Inaelezwa kuwa mara baada aya kukamilika na kuanza rasmi kwa
huduma za matibabu, madaktari wa hapa nchini waliomo katika mgomo na wale zaidi
ya 200 waliodaiwa kufukuzwa na serikali kimyakimya, watalazimika kurejeshwa
kazini kwa masharti makali.
Hata hivyo, uamuzi wa serikali kuwatimua madaktari
wakati suala lao liko mahakamani, umewagawa wabunge.
Baadhi ya wabunge walijaribu kuhoji suala hilo Bungeni,
lakini walikwama baada ya Spika Anna Makinda kuzuia mjadala huo kwa madai
kuwa suala hilo liko mahakamani.
Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala, alisema kuwa
kilichofanywa na serikali ni kiini macho kwani juzi Waziri Mkuu Mizengo
Pinda alisema serikali haiwezi kutoa kauli dhidi ya madaktari kwa
madai kuwa kuna kesi mahakamani.
“Juzi serikali imesema kuwa haiwezi kutoa kauli kwa vile
jambo hilo lipo mahakamani, sasa imewezaje kuwafukuza madaktari wakati jambo
lipo mahakamani?” alihoji Dk. Kigwang’ala.
Aliitaka serikali kuondoa kesi hiyo ili kurejesha
majadiliano kwani ndio njia pekee ya kukabiliana na mgogoro huo.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alimshangaa Spika Anna
Makinda kuzuia mjadala huo kwani ungeweza kujadiliwa bila kuingilia uhuru wa
mahakama.
Juzi uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili,
uliwafukuza kazi madaktari 229 walioko katika mafunzo kwa njia ya vitendo
kutokana na mgomo unaoendelea wa kushinikiza kulipwa posho zao za mwezi
mmoja.
Hospitali zingine ambako madaktari wamefukuzwa kutokana na
mgomo huo ni pamoja na Mbeya na Dodoma.
Jeshi lachukua nafasi za madaktari
Wakati huo huo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
limeanza kutekeleza kwa vitendo agizo la serikali la kutoa huduma za kitabibu
kwa wagonjwa kufuatia mgomo wa madaktari nchini.
Juzi Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwa bungeni alisema
serikali imeamua kuwatumia madaktari waliopo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
wastaafu na hospitali zote za jeshi kuendelea kutoa huduma ya matibabu kwa
wagonjwa.
Msemaji wa JWTZ Kanali Kapambala Mgawe katika mahojiano
maalum na gazeti hili, alisema juzi baada ya Waziri Mkuu Pinda kutoa agizo
hilo, walianza utekelezaji wake ambapo kwa jiji la Dar es Salaam, hospitali Kuu
ya Jeshi Lugalo Kikosi ya 521, Mgulani na ile ya Kikosi cha Navy-Kigamboni na
hospitali zake zote kote nchini zilianza kutoa huduma hiyo bila vikwazo.
“Kwanza naomba umma uelewe hivi hospitali za JWTZ hapa
nchini kwa asilimia 70 zimekuwa zikiwatibu raia bila vikwazo vyovyote hivyo agizo
hilo la serikali huenda likaongeza idadi ya wagonjwa kutibiwa katika hospitali
zetu labda kwa asilimia 90.
Mgawe alisema madaktari wanajeshi wapo kwa ajili ya kulinda
taifa na watu wake, hivyo akawahakikishia wananchi wanaougua kutosita kwenda
katika hospitali za jeshi hilo kutibiwa akidai kuwa hawaoni mantiki ya daktari
kugoma.
No comments:
Post a Comment