Boniface Meena na Aidan Mhando
HATIMAYE
Rais Jakaya Kikwete amesikiliza kilio cha wabunge, vyama vya siasa,
wananchi wa kawaida na wanaharakati kutaka mawaziri waliohusishwa na
kashfa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) wajiuzulu baada ya kukubali kulisuka upya baraza lake.
Taarifa ya Rais Kikwete kutaka kulisuka upya Baraza la Mawaziri ilitangazwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipokutana na waandishi wa habari, Dar es Salaam muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya CCM.
Taarifa ya Rais Kikwete kutaka kulisuka upya Baraza la Mawaziri ilitangazwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipokutana na waandishi wa habari, Dar es Salaam muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya CCM.
Mawaziri ambao wizara zao
zilibainika kuwa na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma katika ripoti
hiyo ya CAG na hivyo kushinikizwa kujiuzulu ni Waziri wa Nishati na
Madini, William Ngeleja; Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu; Waziri wa
Fedha; Mustafa Mkulo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi,
George Mkuchika.
Wengine ni Waziri wa Maliasili
na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji
Mponda na Waziri wa Viwanda na Biashara; Dk Cyril Chami.
Nape alisema Kamati Kuu
iliyokutana jana ilipokea taarifa mbili ikiwemo uamuzi huo wa Rais
kulisuka upya baraza la mawaziri kutokana na ripoti ya CAG.
“Kamati Kuu imepokea taarifa
kubwa mbili, taarifa ya Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM na Kamati ya
Wabunge wa CCM kwa upande mmoja na taarifa ya Kamati ya Uongozi ya
Wawakilishi wa CCM kwa Bara na Zanzibar,” alisema Nape.
Alisema pamoja na taarifa hizo,
Kamati Kuu ilipokea taarifa ya jinsi Rais alivyopanga kuchukua hatua za
kuwawajibisha mawaziri na watendaji serikalini na viongozi wa mashirika
ya umma waliobainika kuhusika na ubadhirifu ulioainishwa na CAG, kamati
za kudumu za Bunge na wabunge.
“Kamati Kuu inatambua na
kuheshimu haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa Serikali yao.
Inapongeza juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa
kwa uwazi na hivyo kuibua upungufu uliojadiliwa,” alisema Nape.
Alisema kutokana na hilo, Kamati
Kuu imeridhika na imebariki uamuzi wa Rais kulisuka upya baraza la
mawaziri na taasisi nyingine zilizoainishwa katika ripoti hiyo ya CAG.
“Kamati Kuu imesisitiza utekelezaji wa
uamuzi huo wa Rais ufanywe mapema iwezekanavyo," alisema na kuongeza
kwamba Rais anaweza kuwabadilisha mawaziri na kuwawajibisha wale ambao
kutokana na uzito wa tuhuma zilizopo kwenye ripoti ya CAG, wanapaswa
kuwajibishwa.
"Taarifa ya CAG ndiyo ambayo ukiipitia inaonyesha nani atawajibishwa kutokana na uzito wa tuhuma,” alisema Nape.
Alipoulizwa lini Rais amepanga kulisuka baraza hilo la mawaziri, Nape alijibu: “Wakati wowote na haraka iwezekanavyo.”
Alisema kabla ya Rais kutoa
uamuzi huo, alikutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juzi ambaye alimpa
ripoti nzima ya mambo yaliyojiri bungeni.
Alisema CCM hakijatikiswa na
sakata la mawaziri hao na kwamba suala lililopo mbele yao ni
kuwawajibisha... “Tunajivunia tumelifikisha suala hili hapa kutokana na
mfumo."
Katika Mkutano wa Saba wa Bunge
la 10 mawaziri hao walishinikizwa wajiuzulu kiasi cha wabunge kumkalia
kooni Waziri Mkuu, Pinda baada ya ripoti hiyo ya CAG kubainisha
ubadhirifu wa fedha za umma kama ilivyowasilishwa bungeni na wenyeviti
wa kamati za tatu za Bunge.
Taarifa za ndani ambazo
zilipatikana baada ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika Dodoma
zilieleza kuwa wabunge wa chama hicho waliagiza mawaziri hao wajiuzulu
kutokana na kushindwa kufanya kazi zao kikamilifu.
Baada ya kikao hicho Katibu wa
Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama aliwaambia waandishi wa habari kuwa
wamekubaliana kwamba uamuzi uliofikiwa katika kikao cha wabunge wa CCM
ungetolewa baadaye na Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda.
Vyanzo vya ndani ya kikao hicho
vilimnukuu Pinda akiwataarifu wabunge kwamba mawaziri wanane walitakiwa
kuandika barua za kuachia nafasi zao.
Chami ajikosha
Wakati akiwa amekalia kuti kavu,
Dk Chami amesema amemwandikia barua Rais Kikwete akitaka amwajibishe
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege.
Hatua
hiyo ya Dk Chami imekuja baada ya wabunge kuchachamaa bungeni wakitaka
Waziri Chami ajiuzulu kwa kile kinachodaiwa kumkingia kifua mkurugenzi
huyo.
Licha ya shinikizo hilo, Waziri
Chami alikuwa akijitetea kuwa asingeweza kumchukulia hatua mkurugenzi
huyo bila kuwa na tuhuma ambazo zingempa nguvu ya kumshauri Rais.
Dk Chami alikuwa akisema kuwa
hadi bunge linamalizika mjini Dodoma wiki hii alikuwa hajaiona ripoti ya
Kamati Ndogo ya Bunge iliyomchunguza Ekelege ambayo ingemsaidia kupata
tuhuma zinazomkabili.
“Hata ripoti maalumu ya ukaguzi
iliyofanywa na CAG mpaka wabunge wanapaza sauti pale bungeni sikuwa
nimeiona na Ekelege ni mteule wa Rais nitamwambia Rais amefanya nini?”
Mkurugenzi huyo mkuu anatuhumiwa
kuisababishia Serikali hasara ya Sh18 bilioni kutokana na utendaji
mbovu katika kusimamia ukaguzi wa magari yanayoingia nchini uliokuwa
ukifanywa na mawakala nje ya nchi.
Dk Chami alithibitisha jana kuwa
baada ya kupokea taarifa ya CAG Aprili 18, mwaka huu siku iliyofuata
alimwandikia barua Rais akimuomba amsimamishwe kazi Ekelege.
Alisema amemuomba Rais afanye
mambo mawili, kumpa likizo ya malipo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma
zinazomkabili na pia airuhusu Bodi ya Wakurugenzi kuteua kaimu katibu
wake.
LHRC nao washinikiza
Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) jana asubuhi kiliitisha mkutano na waandishi wa habari
na kumtaka Rais Kikwete awawajibishe mawaziri wote na watendaji wa
Serikali wanaohusika katika tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk
Hellen Kijo-Bisimba alisema baada ya uchunguzi wa CAG kubaini kuwepo kwa
matumizi mabaya ya fedha za umma, ni wakati wa Rais Kikwete kufanya
uamuzi wa haraka ya kuwawajibisha wote waliohusika.
“Kwa sasa tunaona wazi kwamba
deni la taifa limeongezeka kutoka Sh10.5 trilioni mwaka 2010/2011 na
mpaka kufikia mwaka deni hilo limeongezeka mpaka Sh14.4 trilioni na
kwamba bado kuna misamaha ya kodi kiasi cha Sh1.02 trilioni jambo ambalo
ni la hatari kwa uchumi wa taifa,” alisema Bisimba na kuongeza:
“Kama fedha hizi zingepata
usimamizi mzuri, zingeweza kujenga kilometa 1,000 za barabara bila
kuomba misaada kutoka kwa wafadhili. Jambo jingine la kushangaza ni
kuwepo kwa mishahara hewa iliyolipwa kwa walimu wa vyuo vikuu 17 ambapo
Serikali imepoteza Sh1.9 bilioni ambazo zingeweza kutumika kuwakopesha
wanafunzi zaidi ya 1,000.”
“Tunamuomba Rais Kikwete
alitilie uzito suala hili kwani kuna mambo mengi yamejitokeza wazi na
kuonyesha kwamba mawaziri wake siyo watendaji makini kwani imefikia
wakati wao kwa wao wanatofautiana katika uamuzi jambo ambalo sisi kama
Watanzania linatushangaza.”
“Tumeshangazwa sana kuona utovu
uliokithiri wa nidhamu na kukosekana kwa uwajibikaji unaofanywa na
mawaziri kwani wamekuwa wakitofautiana wao kwa wao jambo ambalo hata
viongozi wa juu kama Waziri Mkuu wamelinyamazia bila kuchukua hatua
zozote hali ambayo inazidi kutuchanganya.”
Bisimba alizipongeza Kamati za
Bunge kwa kile alichoeleza kuwa zimefanya kazi yake vizuri na kusaidia
kufichua baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yamejificha.
“Tukiwa watetezi wa haki za
binadamu tunajiuliza kwamba mawaziri hawa walikuwa wapi kipindi chote
hicho mpaka wabunge wasimame ndipo wawajibike?” alisema.
Aliwataka wabunge kutanguliza
mbele maslahi ya wananchi waliowaweka madarakani na badala ya kujali
maslahi ya vyama vyao au ya mtu binafsi.
Kamati Kuu Chadema
Kwa upande wake, Kamati Kuu ya
Chadema nayo ilikutana Mbezi Beach, Dar es Salaam jana ambako pamoja na
mambo mengine, ilijadili namna itakavyoendesha maandamano nchi nzima
kumshinikiza Rais Kikwete awawajibishe mawaziri hao.
Baadhi ya vyama vya siasa na
taasisi nyingine zimeshaweka bayana msimamo wake wa kuungana na Chadema
katika maandamano hayo. Hizo ni pamoja na Chama Cha Wananchi (CUF),
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na baadhi ya
viongozi wa dini, wasomi na wanaharakati.
No comments:
Post a Comment