(Mama wa marehemu Steven Kanumba, Bi. Flora Mutegoa.)
Habari na Gazeti la Mwananchi
Wiki mbili baada ya kifo cha
aliyekuwa msanii nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba, wazazi wake;
Charles Musekwa Kanumba na Mama yake, Flora Mutegoa ambao hawaishi
pamoja, wametofautiana kuhusu suala la mali na mirathi.
Juzi, Mzee Kanumba aliibuka na
kudai kuwa kuna kundi la watu linalomdanganya mama huyo wa marehemu
kwamba linajua zilipo mali za Steven jambo ambalo alisema ni uongo na
kumtaka awe na subira na asidanganyike.
Hata hivyo, kauli hiyo imepingwa
na Mutegoa ambaye amehoji sababu za mumewe huyo kuzungumzia mali za
mwanaye wakati huu. Alidai kuwa Mzee Kanumba hajawahi kuwa na
mawasiliano na marehemu tangu mwaka 1999 alipoondoka kwao, Shinyanga.
Akizungumza katika mahojiano
maalumu na gazeti hili juzi, Mzee Kanumba alimsihi mkewe kutodanganyika
kwa kuwa yeye akiwa baba mzazi wa Kanumba anajua mali zote za mtoto wake
na ndiye pekee anayeweza kumtendea haki katika kuzigawa.
“Mali za marehemu mwanangu
nazifahamu zote, kwa hiyo hakuna shaka tutazigawa kwa sababu hakuna baba
mwingine na haki yangu ipo palepale hakuna atakayeinyang’anya,” alisema
na kuongeza:
“Nisingependa tuwape watu faida ya
kuanza kuvutana mahakamani, tunatakiwa suala hili tulimalize sisi
wenyewe kama tulivyompata mtoto wetu. Ninasisitiza mali zote zisifanyiwe
vurugu ziachwe kama zilivyo.”
Katika
kuthibitisha kwamba anazijua mali hizo, mzee huyo alisema Steven
ameacha magari matatu, Sh40 milioni, viwanja viwili na akaunti mbili za
benki na Kampuni ya Filamu.
Akerwa na tambiko
Mzee
Kanumba alisema anasikitishwa na tambiko la Kihaya lililofanyika katika
kaburi la mtoto wake, jambo ambalo alisema halikutakiwa kwa kuwa
marehemu alikuwa Mkristo na alizikwa kwa imani hiyo.
“Mimi ni Mkristo, mtu aliyezikwa
Kikristo huwezi tena kuanza kumfanyia mambo ya kipagani na kuanza
kumtambikia, hiyo kwetu hairuhusiwi,” alisema Mzee Kanumba na kuongeza:
“Hata hivyo, marehemu alikuwa
Msukuma, si Mhaya, itakuwaje wamtambikie Kihaya na kumwaga pombe aina ya
rubisi huku marehemu alikuwa hatumii pombe na mimi pia situmii pombe?”
Kuhusu tambiko, Flora alisema
hakuna kitu kama hicho kilichofanyika kwenye kaburi la mwanaye isipokuwa
Wahaya wana mila zao kwa mwenzao aliyepatwa na msiba.
“Kilichofanyika siyo tambiko
bali, ni mila zetu za Kihaya. Unapofiwa wenzako wanakuletea vitu kama
kreti ya soda, bia na mkungu wa ndizi. Lile siyo tambiko ni mila tu,
mimi pia ni Mkristo, siwezi kushiriki matambiko,” alisema.
Alisema suala hilo la kugawa
mali au msimamizi wa mirathi walitakiwa kukutana pande mbili, yaani yeye
na mkewe baada ya kupita siku 20 tangu alipozikwa waangalie namna ya
kugawa huku akisisitiza kuwa hakuna mtu mwingine anayeruhusiwa kuingilia
masuala hayo.
Mama amkana
Kwa
upande wake, Mutegoa ambaye sasa bado yupo nyumbani kwa Kanumba, Sinza
Vatican, Dar es Salaam alisisitiza kwamba marehemu hajawahi kuwasiliana
na baba yake huyo tangu mwaka 1999.
Alieleza kushangazwa na taarifa
hizo kutoka kwa mzazi mwenzake huyo na kusisitiza kuwa ni mapema mno
kuanza kujadili mali za mtoto.
“Nasikitika kulisema hili kwani
bado niko kwenye msiba wa mwanangu. Hata hivyo, sidhani kama mwenzangu
anajua chochote kuhusu Steven, achilia mbali mali zake, hawajawahi kuwa
na ukaribu mpaka kuweza kujua mali zake,” alisema na kuongeza:
“Hata hivyo, mbona anazungumzia
mali tu, hivi anafahamu kama Steven alikuwa na madeni? Ninamsihi aachane
na hizo habari kwa wakati huu kwani hazina uzito wowote ukilinganisha
na thamani ya mtoto niliyempoteza,” alisema.