Source; Francis Godwin
Habari
ambayo imetua hivi punde katika mtandao huu
www.francisgodwin.blogspot.com inadai kuwa serikali imetoa matangazo
rasmi ya Serikali (Government Notices) kuhusu uanzishaji wa mikoa mipya
minne na wilaya mpya 19 ambayo yamechapishwa tangu Machi 2, mwaka huu.
Waziri
Mkuu Mizengo Pinda amesema matangazo hayo ambayo yalisainiwa na Rais
Jakaya Kikwete tangu Machi mosi, 2012, yanabainisha mikoa mipya kuwa ni
Geita, Katavi, Njombe na Simiyu. Mikoa hii imechapishwa katika Tangazo
la Serikali Na. 72.
Wilaya
19 ambazo zimeanzishwa na kuchapishwa katika Tangazo la Serikali Na.73
ni Buhigwe, Busega, Butiama, Chemba, Gairo, Ikungi na Itilima. Wilaya
nyingine ni Kakonko, Kalambo, Kaliua, Kyerwa, Mbogwe, Mkalama na Mlele.
Nyingine ni Momba, Nyang’hwale, Nyasa, Uvinza na Wanging’ombe.
Kwa
mujibu wa matangazo hayo makao makuu ya mikoa hiyo mipya minne yatakuwa
kama ifuatavyo: Geita (Geita), Simiyu (Bariadi) Njombe (Njombe) na
Katavi (Mpanda).
Mikoa hiyo itakuwa na wilaya zifuatazo; Geita utakuwa na wilaya tano za Bukombe, Chato, Geita, Mbongwe na Nyang’hwale. Mkoa wa Katavi utakuwa na wilaya mbili za Mlele na Mpanda. Mkoa wa Njombe utakuwa na wilaya nne za Makete, Njombe, Ludewa na Wanging’ombe wakati mkoa wa Simiyu utakuwa na wilaya tano za Bariadi, Busega, Maswa, Meatu na Itilima.
Makao
makuu ya wilaya mpya zilizoanzishwa ni kama ifuatavyo: Buhigwe
(Buhigwe); Busega (Nyashimo); Butiama (Butiama); Chemba (Chemba); Gairo
(Gairo); Ikungi (Ikungi) Itilima (Lagangabilili); Kakonko (Kakonko);
Kalambo (Matai) na Kaliua (Kaliua).
Nyingine
ni Kyerwa (Rubwera); Mbogwe (Mbogwe); Mkalama (Nduguti); Mlele
(Inyonga); Momba (Chitete); Nyang’hwale (Kharumwa); Nyasa (Mbamba Bay);
Uvinza (Lugufu) na Igwachanya (Wanging’ombe).
Julai
2010, kabla Rais Kikwete hajatoa hotuba ya kulivunja Bunge, Serikali
ilitoa uamuzi wa kuunda mikoa mipya minne na wilaya mpya 21. Hata hivyo,
baada ya kuhakiki mipaka ya maeneo hayo yote na kuandaa maelezo ya mipaka hiyo vizuri (boundary descriptions), wilaya zilipunguzwa na kubakia 19.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, MACHI 8, 2012.
Irene K. Bwire,
Email: irenekaki@yahoo.com