Haki
ya wanawake kushiriki katika maisha ya kisiasa imesisitizwa katika
mikataba kadhaa ya kimataifa, lakini kuibadilisha haki kutoka kwa
maandiko hadi kwenye vitendo kunahitaji jitihada zaidi miongoni mwa
wahusika.
Kulingana na ripoti mpya ya
utafiti iliyochapishwa kwa ushirikiano wa Shirika la Mpango wa Maendeleo
la Umoja wa Mataifa – UNDP na Taasisi ya Taifa ya Demokrasia kwa
Masuala ya Kimataifa, ni kwamba ijapokuwa asilimia 40 hadi 50 ya
wanachama wa vyama vya kisasa kote ulimwenguni ni wanawake, asilimia 10
pekee ndio inashikilia nyadhifa za uongozi.
Msimamizi wa UNDP Helen Clark
anasema kuwa huku kukiwa na chini ya asilimia 20 ya viti vya bunge
ulimwenguni vinavyokaliwa na wanawake, ni wazi kwamba vyama vya kisiasa
vinahitaji kupiga hatua zaidi na vinahitaji kusaidiwa katika juhudi
hizo, za kuwasaidia wanawake katika kujiimarisha kisiasa.
Ushiriki wa vyama vya siasa ni muhimu kwa wanawake
Naibu Katibu Mkuu wa UN Asha-Rose Migiro,
Mkurugenzi wa Kikundi
cha Jinsia cha Shirika la UNDP Winnie Byanyima ameliambia shirika la
habari la IPS kuwa ikiwa tunataka kueneza demokrasia na kuwapa uwezo
wanawake kisiasa, ni sharti tushirikiane na vyama vya kisiasa. Byanyima ambaye ni mbunge wa zamani wa Uganda na pia mwanadiplomasia aliongeza kuwa Ikiwa wanawake hawapewa uongozi wa vyama vya kisiasa, basi hawawezi kuziongoza serikali.
Kimataifa, idadi ya mawaziri
wanawake serikalini iko chini ikiwa ni kiwango cha wastani cha asilimia
16. Na idadi ya viongozi wanawake wa nchi na serikali bado iko chini, na
imepungua katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa nini chini ya asilimia
tano katika mwaka wa 2011.
Utafiti huo unasema idadi hiyo
ya chini imeendelea kushuhudiwa katika miongo mitatu iliyopita ya
uhamasisho na juhudi za jamii ya kimataifa kuangamiza ubaguzi na kuwapa
uwezo wanawake.
Umoja wa Mataifa watambua jukumu la wanawake
Waziri Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton |
Ijapokuwa kunayo maeneo
yanayojaribu kujizatiti na kutimiza lengo hilo, vizingiti kadhaa vingali
njiani mwa juhudi za wanawake kushiriki kikamilifu kama wagombea.
Kulingana na takwimu za hivi
punde za Chama cha Kimataifa cha Wabunge IPU na Wanawake wa Umoja wa
Mataifa, idadi ya wanawake kama viongozi wa nchi au serikali ni 18 kati
ya nchi 193.
Utafiti huo wa UNDP na NDI
unataja baadhi ya mikakati inayoweza kutumiwa wakati wa uchaguzi, kama
vile kuwapa mafunzo na kuwahimiza wagombea wa kike na kuhakikisha
wanawake wanaonekana kwa wingi katika kampeni.
Wanawake na wanaume wawe katika uwiano sawa kimaendeleo
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Haki za
Binadamu Navi Pillay
|
Shirika la NDI
linasema limefanya kazi na zaidi ya vyama 720 vya kisiasa na mashirika
katika zaidi ya nchi 80 ili kuweka mazingira bora na ya wazi ambapo
wanaume na wanawake wanaweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa
demokrasia.
Katika awamu ya kabla ya
uchaguzi, usajili na uteuzi wa wagombea ni shughuli muhimu zaidi ya
kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki siasa. Lakini pengo la jinsia
hupanuka kwa kiwango kikubwa wakati wagombea wa nyadhifa za kisiasa
wakisonga kutoka hatua ya kuwa halali na kuwa wagombea, na kisha
kuteuliwa na chama kuwa wagombea wa nyadhifa hizo.
Utafiti huo unataja mifano
kadhaa ya usawa wa kijinsia chama kimoja cha kisiasa nchini Canada kina
kamati ya kuwasajili wagombea ili kuhakikisha mchanganyiko katika uteuzi
wa wagombea. Nchini Costa Rica, moja ya vyama vya kisiasa hubadilisha
wagombea wa kiume na kike kwenye orodha ya uchaguzi.
Nchini Afrika Kusini, wanachama
wa kike katika vyama walishinikiza mabadiliko katika ratiba ya bunge ili
kuwajumuisha wabunge wenye familia, na pia wakashinikiza mijadala
kumalizika mapema jioni ili kuwapa nafasi wabunge walio na familia na
kwa vifaa vya malezi ya watoto kuwekwa.
Nchini Ujerumani, chama cha
Christian Democratic Union (CDU) kiliidhinisha asilimia 33 ya viti
maalum vya maafisa wa chama katika mwaka wa 1996. Na ikiwa viti hivyo
maalum havitapatikana, uchaguzi wa ndani sharti urudiwe.
Mwandishi: Bruce Amani/IPS
Mhariri: Josephat Charo