Mtu aliyedai kuwa ni mwanamuziki mashuhuri aliyekufa na kufufuka Afrika Kusini ameshtakiwa kwa udanganyifu, polisi wamesema.
Mtu huyo alisema yeye ni Khulekani "Mgqumeni" Khumalo - mwanamuziki maarufu wa miondoko ya Kizulu ambaye alifariki mwaka 2009. Amedai kuwa alitekwa nyara na mchawi
ambaye alimfanyia mazingara na kumfungia katika pango na mizuka
wengine, vimeripoti vyombo vya habari vya Afrika Kusini.
Lakini polisi wamesema alama za vidole vya mtu huyo vimeonesha sio
mwanamuziki anayedai kuwa, bali jina lake halisi ni Sibusiso John
Gcabashe, mwenye umri wa miaka 28.
"Kufufuka" kwa Khumalo kulizua tafrani na
mashabiki wake kumiminika nyumbani kwake mwishoni mwa wiki, kiasi cha
polisi wa kutuliza ghasia kuitwa na kutumia maji yenye nguvu kudhibiti
umati wa watu.
Mtu huyo aliyejidai "amefufuka" amefikishwa
katika mahakama ya mwanzo ya Nquthu iliyopo Kwazulu-Natal siku ya
Jumanne ambapo ameshtakiwa kwa kosa la udanganyifu. Hakutakiwa kujibu
lolote, amesema msemaji wa polisi Kanali Jay Naicker.
Amesalia rumande hadi Februari 14 ambapo ataruhusiwa kuomba dhamana na pia kusikia kama anakiri au kukana mashtaka yake.
Familia ya marehemu Khumalo ilionekana
kugawanyika kuhusiana hasa na utambulisho kamili wa mtu huyo, huku wake
zake wawili wakisema ni yeye, lakini rafiki wa zamani wa kike wa
mwanamuziki huyo, Zehlise Xulu, akisisitiza kuwa sio mwenyewe.
Bi Xulu ambaye alizaa naye mtoto wa kiume ambaye
ana umri wa miaka 10 sasa, amesema ana matumaini kuwa mtu huyo atakutwa
na hatia na kufungwa jela kwa miaka mingi kutokana na "kurejesha
majonzi ya zamani".
"Mwanangu alisafiri hadi Johannesburg akiwa na
matumaini ya kumuona baba yake, badala yake alikuta mtu mwenyewe ni
mhuni tu," amesema Bi Xulu akikaririwa na gazeti la Mercury.
"Nilikasirishwa sana kila mara alipokuwa akiniita mpenzi wake," amesema.
Imani za uchawi ni jambo la kawaida Afrika Kusini, hasa maeneo ya vijijini.
~BBC
No comments:
Post a Comment