ILIKUNJOMBE ADAI YEYE, MKONO, LUGOLA WALIPONZWA NA PINDA, NAPE ATAKA WASIORIDHIKA WAKATE RUFAA, WASOMI WAPONGEZA
Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kutangaza majina ya
wagombea, baadhi ya vigogo walioachwa kwenye uteuzi huo wameeleza ya
moyoni, huku Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe akisema anaamini
ametoswa kwa sababu alitia saini ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda.
Nimrod Mkono
|
Katika Bunge la 10 lililoketi Aprili mwaka huu, baadhi ya Wabunge wa CCM
akiwamo Filikunjombe, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono na Mbunge
wa Mwibara, Kangi Lugola, waliunga mkono hoja ya kutokuwa na imani na
Pinda iliyokuwa imeanzishwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe wa Chadema.
Wabunge hao wa chama tawala, waliungana na wenzao wa upinzani kutaka
kupiga kura za kutokuwa na imani na Pinda kutokana na kile kilichoelezwa
kuwa ameshindwa kuisimamia Serikali kwa kuwawajibisha mawaziri wazembe.
Hata hivyo, mpango huo haukufanikiwa baada ya Spika wa Bunge Anne Makinda kueleza kuwa haukufuata taratibu zinazotakiwa.
Filikunjombe alipotakiwa jana kuzungumzia kuenguliwa kwake kwenye
kinyang'anyiro cha uchaguzi wa ndani ya chama, alisema anaamini yeye na
wenzake hao wa CCM, wametoswa kwa sababu ya kushiriki mpango wa kumng'oa
Waziri Mkuu Pinda.
Hata hivyo, alisema amelazimika kukubali hali hiyo na kupokea matokeo,
kwa kuwa hatua yake ya kusaini kitabu hicho ilitokana na nia njema
kutaka Waziri Mkuu ajiuzulu ili mambo fulani muhimu katika jamii
yafanyike.
Filikunjombe alibainisha kuwa alisaini kitabu hicho cha kutokuwa na
imani na Pinda akiwa na akili timamu na alikuwa anajua kinachoweza
kutokea kutokana na hatua yake hiyo.
"Nimesaini kitabu kile kwa nia njema, nikiwa na akili timamu na sijutii
uamuzi wangu huo, ila siwezi kuwasemea Kigwangalla (Khamis mbunge wa
Nzega) na Bashe (Hussein). Lakini sisi watatu (yeye, Lugola, Mkono)
tumeenguliwa kwa sababu hiyo (ya kutokuwa na imani na Pinda)."
Aliendelea: "Nashangaa leo naonekana adui wa chama wakati nilikuwa
nakinusuru na kusema kweli adui wa CCM ni Wabunge wa chama hicho ambao
hawakusaini kitabu hicho cha kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, " alisema
Filikunjombe.
Mkono
Mbunge wa Musomo Vijijini, Nimrod Mkono alisema kutoswa kwake ni uamuzi wa watu aliowaita wenye chama.
"Walikata jina langu nikakata rufaa, likarudishwa Dodoma, lakini
walipokutana wakaona sifai. Wakaamua kunifukuza sasa hapo mimi nifanye
nini?" alihoji Mkono.
Mkono alisema huu ni utaratibu wa chama chao cha CCM ambao umewapa
baadhi ya watu haki ya kuwafukuza wengine bila kuwapa fursa ya
kujitetea.
"Kama ilivyotokea kwangu wamekaa na kuona Mkono hafai, fukuza basi
wakafanya hivyo na hiyo haijalishi kama nilisaini kutokuwa na imani na
Waziri Mkuu au la. Suala la msingi ni kuwa Mkono amefukuzwa na atarudi
kama ilivyokuwa kwa mwana mpotevu." alisema bila kufafanua.
Kigwangalla
Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla alisema anaheshimu uamuzi wa vikao
vilivyokaa na kufikia uamuzi uliochukuliwa na kwamba, ataendelea kuwa
mwanachama na kukitumikia chama pamoja na wananchi kwa nguvu zote bila
kinyongo.
“Nitaendelea kuheshimu vikao vya chama changu na kuwa mwanachama hai
ingawa sijajua wametumia vigezo gani kuteua majina hayo,” alisema Dk
Kigwangalla.
Bashe
Kwa upande wake Bashe alisema kilichotokea ni uamuzi wa chama na vikao halali vilivyokaa na kuchukua uamuazi huo.
“Sijui kwa nini jina langu halikupitishwa, lakini nitaendela kuwa
mwanachama na kuwatumikia wananchi wenzangu wa Nzega,” alisema Bashe.
Katika kuhakikisha hilo, Bashe alisema leo anakwenda Nzega kupeleka
mifuko ya saruji tani 18 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za kata za chama
hicho wilayani humo.
Nape ajibu
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alitaka makada
waliotoswa na wenye kinyongo wawasilishe malalamiko yao CCM kwa
maandishi badala ya kulalamika nje ya utaratibu."Wathibitishe kwa
maandishi nasi chama tutajua la kufanya, kwani wabunge hao hawakuingia
katika vikao vilivyotoa maamuzi sasa nashangaa kusikia katika vikao
tuliwajadili na hoja iliyowaondoa ni hiyo," alisema Nape.
Maoni ya wasomi
Wakizungumzia uteuzi huo wasomi na wanasiasa walitoa maoni tofauti huku
baadhi wakisema chama kinatakiwa kuwa na sera na mtizamo wa kuliletea
maendeleo taifa bila kujali kama chama kinaongozwa na wazee au vijana.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema uamuzi
huo wa CCM umeonyesha kuwa, ndani ya chama hicho hakuna aliye juu kuliko
mwenzake.
“Wapo waliosema wakitoswa patachimbika, lakini wametoswa na
hapajachimbika, uamuzi wa kuwatosa watu wa aina hii utarejesha nidhamu
ndani ya chama hicho licha ya kuwa kazi bado ni kubwa,” alisema Dk Bana.
Profesa Gaudence Mpangala alisema vijana kupewa nafasi kubwa ya kugombea
nafasi mbalimbali ndani ya CCM, hakuna maana kuwa sera na mtizamo wa
chama hicho utabadilika.
“Kuwa na wanachama au wagombea wenye umri wa wastani(vijana) sio kigezo
cha chama kufanya vyema kwa sababu hawawezi kubadili sera na mtizamo wa
chama husika,” alisema Mpangala.
Dk Kitila Mkumbo alisema kuingiza vijana wengi katika mpambano huo ni
hatua ya ukomavu wa kisiasa kwa kuwa chama hicho awali hakikuwa na
utaratibu mzuri wa kuwapa nafasi ya uongozi vijana.
“Awali Chadema ndio kilionekana chama kinachowapa nafasi zaidi vijana,
lakini kwa hatua hii ya CCM ni nzuri, sasa tunasubiri utendaji wao kama
utakuwa na manufaa kwa taifa,” alisema Mkumbo.
Bashiru Ally alisema kama kigezo cha kuweka vijana wengi kitazingatia
msimamo, fikra na ufanisi katika utendaji kazi wao basi taifa lina kila
sababu ya kuunga mkono hatua hiyo.
Alisema kwa kuwa vijana ndio chachu ya maendeleo kwa mataifa mbalimbali
duniani, hatua ya CCM kuwapa nafasi vijana ni nzuri kama wakiifanya kazi
hiyo kwa manufaa ya taifa kwanza.
Habari hii imeandikwa na Ibrahim Yamola, Fidelis Butahe, Elizabeth Edward na Joseph Zablon
No comments:
Post a Comment