HOJA ya uteuzi wa majaji wasio na sifa iliyotolewa na Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), imeonekana kuitesa Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge na hivyo kutangaza kuzuia mjadala huo
kwenye vyombo vya habari.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Brigedia Jenerali mstaafu, Hassan Ngwilizi,
jana aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa vyombo vya
habari na jamii hawapaswi kuzungumzia hoja hiyo kwa madai kwamba
kufanya hivyo kunaingilia uhuru wa kamati yake.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo kwa sasa suala hilo bado linashughulikiwa
kamati yake na watakapokamilisha kazi hiyo uamuzi wake utatolewa katika
kikao kijacho cha Bunge.
“Kwa sasa bado kamati yetu inaendelea na uchunguzi kuhusu suala hilo
hivyo basi tunashauri watendaji wa serikali, wa mahakama, vyombo vya
habari na jamii kwa ujumla kutoendelea kujadili ili kuiwezesha kamati
yetu kufanya kazi yake kwa uhuru kama inavyotakiwa,” alisema Ngwilizi.
Aliongeza kuwa kamati inafanya kazi zake kwa usiri na haitakiwi suala
hilo kujadiliwa nje ya Bunge, hivyo kwa wanaoendelea kutoa maoni yao nje
ya Bunge wanakiuka kanuni za uwepo wa kamati hiyo.
Alisema kamati hiyo imekuwa ikishuhudia majadiliano na malumbano makali
yanayoanzishwa kupitia vyombo vya habari kuhusu jambo hilo huku vingine
vikirejea taarifa zinazodaiwa kusemwa ndani ya vikao vya kamati.
Alitoa rai kwa vyombo vya habari au taasisi zinazodhani kuwa zina maoni
kuhusiana na hoja hiyo iliyotolewa na Lissu, kuyawasilisha kwa Katibu wa
Bunge ili ziwasilishwe kwao na kufanyiwa kazi.
Chanzo Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment