Mwandishi Wetu, Dodoma
HALMASHAURI Kuu ya CCM (Nec), imetangaza majina ya wagombea walioteuliwa
kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho, huku
ikionyesha kuwa uchaguzi huo utakuwa na mchuano mkali.
Katika orodha iliyotolewa jana, baadhi ya makada wake maarufu akiwamo
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono na Salum Londa wametupwa.
Mchuano mkali unaonekana kuwapo kwenye nafasi ya ujumbe wa Nec Mkoa wa
Manyara ambako Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye anachuana na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary Nagu.
Mchuano huo unatarajiwa kuwa mkali katika nafasi ya uenyekiti kwenye
baadhi ya mikoa kutokana na kupitishwa kwa majina ya makada wake
maarufu. Mwanza ni miongoni mwa mikoa hiyo kwani Nec imepitisha jina la
Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo ambaye atachuana
na Clement Mabina anayetetea nafasi hiyo.
Makada hao watapata ushindani mkali kutoka kwa Zebedayo Athumani, Joseph Yaredi na Mashimba Hussein Mashimba.
Dar es Salaam nako kunatarajiwa kuwa na mchuano mkali kwani mwenyekiti
wa sasa, John Guninita atachuana na Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi Makao
Makuu ya CCM, Matson Chizzi na kada mwingine, Ramadhan Madabida. Godfrey
Mwalusamba, Harold Adamson na Paul Laizer wanawania nafasi hiyo mkoani
Arusha.
Vita nyingine kali ipo kwenye Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania (UWT),
ambako Mwenyekiti wa sasa, Sofia Simba ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto anachuana na Mbunge wa Same Mashariki, Anna
Kilango Malecela na Mbunge wa Viti Maalumu, Mayrose Majige.
Katika Jumuiya ya Wazazi, Mkono ambaye alikuwa akiwania nafasi hiyo
ametupwa na kuwaacha Abdallah Bulembo, Martha Mlata na kada wa siku
nyingi, John Barongo kuchuana.
Awali, Mkono alikatwa jina lake na Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya hiyo
na kutangaza hali ya hatari akisema asipopitishwa patachimbika. Jina
lake lilirejeshwa na Kamati ya Usalama na Maadili kabla ya kukatwa tena
na Kamati Kuu.
Alipoulizwa jana kuhusu kuondolewa katika kinyang’anyiro hicho, Mkono
alisema: “Nimekubaliana na uamuzi wa chama na nitaendelea kuwa
mwanachama wa CCM. Nimelelewa na kukulia CCM na nitaendelea kubaki CCM
nikiwa mwanachama mtiifu.”
Katika Jumuiya ya Vijana (UVCCM), mchuano mkali unaonekana kuwa katika
nafasi ya makamu mwenyekiti kwani mmoja wa wagombea waliopitishwa, Paul
Makonda anaaminika kuwa na nguvu kubwa kutoka katika kundi la wabunge na
mawaziri wapambanaji wa ufisadi. Makonda anawania nafasi hiyo pamoja na
Mboni Mhita na Ally Hapi.
Nafasi ya Mwenyekiti UVCCM inawaniwa na Sadifa Juma Khamis, Rashid Simai Msaraka na Lulu Mshamu Abdallah.
Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa atachuana
na Dk Salash Toure na Nanai Kanina kwenye nafasi ya ujumbe wa Nec
kupitia Wilaya ya Monduli.
Wagombea wa ‘kundi la kifo’
Vigogo kadhaa wamepitishwa kuwania nafasi 10 za Nec, wakiwamo baadhi ya mawaziri na viongozi wa juu wa chama hicho.
Miongoni mwao ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji,
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo David, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi,
Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe na Katibu Mkuu wa CCM,
Wilson Mukama.
Wengine ni Katibu wa Fedha na Uchumi CCM, Mwigulu Nchemba, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano, Stephen Wassira, Waziri wa Habari,
Michezo, Utamaduni na Vijana, Dk Fenela Mukangara na Katibu Mkuu wa
UVCCM, Martin Shigela.
Kwa upande wa Zanzibar, nafasi 10 za Nec kupitia kapu zinawaniwa na
Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan.
Katika orodha hiyo wamo, Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame
Mnyaa Mbarawa, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi,
Waziri wa zamani wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, Mohamed Seif
Khatib, Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Omar Yussuf Mzee na
Naibu Waziri wa Fedha wa zamani, Abdisalami Issa Khatib.
Familia ya Kikwete
Katika uteuzi huo wa wagombea, majina matatu ya wagombea kutoka katika familia ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete yamepitishwa.
Waliopitishwa ni pamoja na mkewe Salma Kikwete ambaye anakuwa mgombea
pekee katika nafasi ya ujumbe wa Nec Lindi Mjini na Ridhiwan Kikwete
ambaye pia ni mgombea pekee wa nafasi hiyo katika Wilaya ya Bagamoyo.
Mbali ya hao, Nec pia imepitisha jina la Mohamed Mrisho Kikwete kuwania nafasi ya uenyekiti wa Wilaya ya Bagamoyo.
Vigogo watemwa
Nec imewatema vigogo kadhaa, baadhi yao ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Kigoma, Azim Premji na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro,
Vicky Nsilo-Swai ambaye alikuwa anagombea ujumbe wa Nec kupitia Wilaya
ya Hai na kada wa siku nyingi, Salum Londa.
Pia wamo wabunge, Sarah Msafiri, Munde Tambwe, Deo Filikunjombe na
Victor Mwambalaswa.Wengine waliotemwa ni Hussein Bashe na hasimu wake
mkubwa kisiasa Dk Hamis Kigwangalla, Jamali Kassim, Anthony Mavunde na
Emmanuel Nzungu, ambaye aliomba kugombea Uenyekiti Wilaya ya Ilemela,
Mwanza.
Mgeja chupuchupu
Mwenyekiti wa sasa wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja aliponea
chupuchupu kutemwa baada ya Nec kurejesha jina lake kwenye orodha ya
wagombea lililokuwa limeondolewa na vikao vya awali.Taarifa za
kuondolewa jina la Mgeja zilivuja tangu juzi wakati kikao cha Kamati Kuu
kilipoketi ikidaiwa ni kutokana na malumbano kati yake na Mbunge wa
Kahama, James Lembeli.
Inadaiwa wakati wa kujadiliwa Mgeja, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete alitoka kwenye kikao na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
na kumwachia kiti Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa.
Baada ya mjadala mrefu wa kumtetea Mgeja kwamba hakutendewa haki, Msekwa alifikia uamuzi wa kurejesha jina.
“Baadhi ya waliomtetea ninaokumbuka ni Dk Makongoro Mahanga na Peter
Serukamba, lakini wakati wa mjadala wa Mgeja, Mwenyekiti (Kikwete) na
Nape walikwenda chemba, kiti akaachiwa Msekwa,” kilisema chanzo chetu.
Awali, kada mkongwe wa chama hicho, Kingunge Ngombale - Mwiru aliituhumu
Kamati Kuu kwamba imevunja kanuni za uchaguzi kwa kuteua majina zaidi
ya matatu kwenye nafasi moja.
Hata hivyo, inadaiwa Msekwa alimsomea kanuni moja baada ya nyingine
zinazohusu uteuzi hali iliyoonyesha kama kumweka darasani na hatimaye
ikabainika hakuna kanuni iliyovunjwa.Hoja hiyo ilitokana na baadhi ya
mikoa kwenye nafasi moja kusimamisha wagombea zaidi ya watatu kama
nafasi ya mwenyekiti mkoa wa Mwanza.
Hatua hiyo inadaiwa inalenga kuondoa matokeo ya kupanga kwa baadhi ya
wagombea na kwamba, kwa hali hiyo mshindi hawezi kupatikana kwa mzunguko
wa kwanza.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba
anadaiwa kushambulia mtandao uliokuwa umejipanga na kuweka wagombea wao
hata kama hawana sifa.“Yule mzee (Makamba) amewachana-chana vibaya,
anasema hapa tunasajili timu, kama majina hayafai yaondolewe,”
kilidokeza chanzo na kuongeza kwamba hoja hiyo iliungwa mkono na kada
mkongwe wa chama hicho, Mzee Peter Kisumo.
No comments:
Post a Comment