SERIKALI imesema katika mwaka huu wa fedha, itatengeneza
ajira 800,000 katika fani mbalimbali nchini.
Kauli hiyo ya serikali ilitolewa bungeni jana na Waziri wa
Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na
matumizi kwa wizara yake kwa mwaka 2012/2013.
Alisema fursa za ajira hizo mpya zitapatikana kupitia miradi
ya maendeleo chini ya mpango wa taifa wa miaka mitano unaotekelezwa na wizara
na taasisi mbalimbali ((FYDP I).
“Takwimu hizi ni mbali na ajira za watumishi 56,678
watakaoajiriwa na serikali kama ilivyobainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ” alisema.
Waziri Kabaka alisema ajira hizo zitapatikana katika sekta
za kilimo, ujenzi, mawasiliano na viwanda.
“Ajira zitakazozalishwa katika Kilimo ni 169,189, ujenzi wa
miundombinu ya barabara 646,615, mawasiliano 27,600 na katika sekta ya viwanda
na biashara zitazalishwa ajira 5,000,” alisema.
Alibainisha kuwa katika mpango huo wa kuongeza ajira,
halmashauri za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani zitazalisha ajira 6,885.
Alieleza kuwa katika mwaka wa fedha ulioisha, jumla ya ajira
250,678 zilipatikana kutokana na miradi ya maendeleo.
Alisema ajira zilizopatikana katika miradi mbalimbali
ikiwemo Tasaf (34,516), ujenzi wa barabara (42,107) na ujenzi wa majengo ya
serikali (17,685).
Miradi mingine kituo cha taifa cha uwekezaji (TIC) ajira
82,834, mamlaka ya ukanda wa kiuchumi (EPZA) 15,100 na serikali ilitengeneza
ajira 38,289.
Source: tanzania daima
No comments:
Post a Comment