MWANDISHI WA BBC AMSHUHUDIA AKIPUMULIA MASHINE KATIKA HOSPITALI MOJA AFRIKA KUSINI, MKUU WA JOPO LA MADAKTARI ALIYEMTIBU DAR AONGEA
Dk Ulimboka
Waandishi Wetu, Dar na Afrika Kusini
AFYA ya Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka aliyeanza matibabu akiwa chini ya uangalizi maalumu wa madaktari (ICU), baada ya kutekwa, kupigwa na kisha kutupwa kwenye pori la Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ni mbaya, Mwananchi limeelezwa.Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa daktari huyo wa magonjwa ya binadamu, sasa hajitambui na anapumulia mashine katika moja ya hospitali za nchini Afrika Kusini alikolazwa kwa matibabu hayo.
Dk Ulimboka ambaye awali kulizuka utata wa mahali alipo; Afrika Kusini au Ujerumani, sasa imethibitika kuwa yuko Afrika Kusini, lakini hali yake ni mbaya.
"Ukweli ni kwamba yuko Afrika Kusini, lakini taarifa tulizozipata leo (jana) asubuhi ni kwamba sasa amelazwa ICU akiwa hajitambui kabisa," alisema mmoja wa madaktari wanaofuatilia kwa karibu matibabu ya Ulimboka.
Aliendelea, "Sasa hajitambui na tumwombe Mungu tu afanye miujiza yake."
Kiongozi wa Jopo la Madaktari linaloshughulikia matibabu ya Dk Ulinboka, Profesa Joseph Kahama alisema amezisikia taarifa hizo zikitangazwa na Kituo cha Utangazaji cha Uingereza, (BBC) jana asubuhi, lakini hajaweza kuzithibitisha.
"Asubuhi wote tulisikia kwamba hali yake (Dk Ulimboka) ni mbaya na yuko kwenye 'koma', lakini taarifa hizo sijazithibitisha kujua zina ukweli kiasi gani," alisema.
Mwananchi liliwasiliana na mwandishi wa BBC Afrika Kusini, Omary Mutasa ambaye alisema kwamba, ni kweli alikwenda kwenye hospitali (jina linahifadhiwa kwa sasa) alikolazwa Dk Ulimboka ambako alimkuta akipumua kwa usaidizi wa mashine na alikuwa hawezi kuongea.
“Niliingia hadi sehemu alikolazwa Dk Ulimboka, nimeona akipumua kwa usaidizi wa mashine, hata ndugu zake walishtuka sana kuniona pale na hawakufurahishwa mimi kwenda pale,” alisema katika mahojiano ya simu na Mwananchi.
Mutasa alisema kwamba, jana jioni alikwenda hospitali kuangalia hali yake inaendeleaje, lakini hakuweza kumwona.
“Nimejaribu kwenda tena jioni kupata taarifa za hali yake, lakini nimeshindwa kumwona. Utawala wa hospitali ulinikatalia kabisa,” alisema.
Jana asubuhi, Mutasa aliripoti katika kipindi cha asubuhi cha BBC kwamba hali ya Dk Ulimboka ni mbaya na kalazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi na anapumulia mashine.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Madaktari (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema haelewi uvumi huo umetoka wapi kwani yeye hana taarifa hizo.
“Mimi bado nashindwa kuelewa kwani nimezungumza na na wenzangu ambao wanawasiliana na ndugu wa Dk Ulimboka kwa karibu wakasema hakuna taarifa zozote zile mbaya,” alisema Dk Kabangila.
Naye Rais wa Chama hicho, Dk Namala Mkopi alisema hajawasiliana na Dk Ulimboka tangu juzi.
“Bado sijawasiliana na Dk Ulimboka na hatujapata taarifa zozote za hali yake kama ni mbaya au vipi,” alisema Dk Mkopi.
Mbowe ataka uchunguzi
Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ameitaka Serikali kuifanyia kazi Sheria ya Uchunguzi wa vifo vyenye utata kama ilivyoahidiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kikao cha bajeti mwaka jana.
Akizungumza katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu, Mbowe alisema kutotimizwa kwa ahadi hiyo kunaleta hisia kwamba Serikali inahusika katika baadhi ya vifo hivyo.
Mbowe alisema kuwapo kwa vifo vya aina hiyo nchini huku baadhi yake vikihusishwa na vyombo vya dola, kunahitaji uchunguzi wa kina na yakinifu utakaofanywa na chombo huru ili kubaini wahusika na kisha kuwachukulia hatua za kisheria.
“Katika hotuba yako Waziri Mkuu ulikiri kuwepo kwa tatizo hilo na ulisema sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata itafanyiwa kazi na vifo vyenye utata vitafanyiwa uchunguzi, pengine unaweza kutwambia ni upi utekelezaji wa ahadi yao hiyo?” alisema Mbowe wakati anamwuliza swali Waziri Mkuu.
Mbowe alisema hisia za dola kuhusika katika mauaji na mateso haya ya raia zimekuwa zikikuwa kila kukicha na hivyo taifa limepata sifa mbaya katika anga za kimataifa hasa baada ya kipigo cha Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka na wabunge wa Chadema jijini Mwanza.
Akijibu swali hilo Waziri Pinda alisema si kweli kuwa taifa linapata sifa mbaya kutokana na tukio la kupigwa kwa Dk Ulimboka.
“Sikubaliani na hoja kuwa sifa ya nchi imeharibika. Kwa lipi? Ukisema hivyo uwe na ushahidi wa hilo. Vilevile ukitumia mfano wa Ulimboka si mzuri. Jambo hili linahitaji kupatikana ukweli kwanza. Sasa tumeagiza uchunguzi wa kina na wa haraka kufanyike ili tupate ukweli huo,” alisema Pinda.
Kuhusu sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata, Waziri Mkuu Pinda alisema ni kweli aliahidi kwamba sheria inahitaji kufanyiwa marekebisho na kwamba tayari vyombo husika vimepewa maelezo ili kuwezesha mabadiliko hayo kufanyika.
“Wakati mwingine ni uzembe na ufuatiliaji duni. Si kweli kuwa Serikali inahusika. Sisi (Serikali) tutaendelea kufuatilia jambo hilo kwa umakini na kuhakikisha sheria hiyo inaanza kufanya kazi,” alisema Pinda.
Habari hii imeandaliwa na Ibrahim Yamola, Fredy Azzah, Florence Majani, Dodoma
No comments:
Post a Comment