Na Mwinyi Sadallah Zanzibar
Bajeti ya Wizara ya Nchi Ofisi
ya Rais (Ikulu) Zanzibar imepita kwa mbinde, baada ya vifungu vingi vya
matumizi ya fedha kukosa maelezo ya kina na kulazimika wajumbe kuzuia
matumizi ya Sh. milioni 190 katika bajeti hiyo.
Hali hiyo imejitokeza wakati
Baraza la Wawalikishi (BLW) lilipokaa kama kamati ya matumizi kupitisha
vifungu vya bajeti hiyo chini ya Mwenyekiti wake Spika wa Baraza hilo,
Pandu Ameir Kificho.
Fedha zilizozuiwa na wajumbe ni
Sh. milioni 50 ambazo zilikuwa zitumike kununua televisheni kwa matumizi
ya Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Sh. milioni 150 ambazo
zilikuwa zitumike katika mradi wa kilimo wa ushirikiano kati ya serikali
ya Zanzibar na Misri mwaka huu.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji
Mkongwe (CUF), Ismail Jussa Ladhu, alisema kwamba haiwezekani Sh.
milioni 40 kutumika kwa manunuzi ya seti za televisheni wakati huduma
nyingi zinakabiliwa na matatizo na kutaka fedha hizo zisipitishwe.
Hata hivyo Waziri mwenye dhamana
wa Wizara hiyo, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, alisema kwamba wakati wa
kutayalisha bajeti hiyo walikosea fedha hiyo imekusudiwa kununua
jenereta na siyo televisheni.
Kutokana na utata huo Baraza
liliamua kutopitisha kifungu hicho cha matumizi na kuwataka watendaji
wakuu wa serikali kuwa makini wanapotayarisha bajeti za serikali.
Aidha, wajumbe hao pia
wamesitisha matumizi ya Sh. milioni 150 ya utekelezaji wa mradi wa
kilimo cha mbogamboga wa ushirikiano kati ya serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na Serikali ya Misri.
Mwakilishi wa Jimbo la Mkwajuni
Mbarouk (CCM), Wadi Mussa, alisema kwamba tangu mradi huo ulipoazishwa
SMZ imekuwa hainufaiki na tayari Sh. bilioni moja zimetumika katika
uendelezaji wa mradi huo.
Alisema hakubaliani na
kuidhinishwa kwa Sh. milioni 300 wakati mazao yanayozalishwa katika
shamba hilo yamekuwa yakivunwa na kusafirishwa kwenda Misri bila ya
Zanzibar kunufaika na mradi huo.
Akishagiliwa na wajumbe alisema
kwamba Kamati ya Fedha na Uchumi ilipotembelea mradi huo imegundua hata
mkataba wake hauna tija kwa Zanzibar na umelenga kuipatia shamba la
kilimo serikali ya Misri visiwani humo.
Hata hivyo Waziri Mwinyihaji,
alisema kwamba mradi huo lengo lake kubwa ni kufanya utafiti wa mbengu
za mazao tofauti na jina linalotumika katika mkataba wa mradi, jambo
ambalo lilipingwa na wajumbe wa baraza hilo.
Mwakilishi huyo alisema kwamba
kazi za utafiti wa mbegu na mazao zinatakiwa kufanywa na wanasayansi
wakiwemo wataalamu wa kilimo na siyo askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi
ambao wamepewa kazi ya utekelezaji wa mradi huo.
Kutokana na utata wa maelezo ya
Waziri, wajumbe wa baraza hilo kwa kauli moja waliamua fedha hizo
kusitishwa matumizi yake hadi tathimini ya mradi huo itakapofanyika
kuangalia faida na hasara yake.
Maeneo mengine yaliyotaka
kuikwamisha bajeti hiyo ni matumizi ya Sh. milioni 110 yaliyopangwa
kutumika katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya viburudisho katika Idara
ya Utumishi na Uendeshaji kutoka Sh. milioni 6 katika bajeti ya mwaka
jana.
Aidha, Jussa alitaka kujua kwa
nini bajeti hiyo imejaa vifungu vya matumizi ya fedha na kupewa jina la
posho maalum huku kukiwa hakuna maelezo juu ya watu watakaonufaika na
posho hilo.
Jussa, pia alipinga matumizi ya
Sh. milioni Sh. 337.5 fedha ambazo zimependekezwa kutumika kama ada ya
mikataba katika idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari mkazi
katika mwaka huu wa fedha.
Wajumbe wengine waliyozuia
vifungu vya bajeti hiyo ya Ikulu, ni Asha Bakari Makame, (Viti Maalum)
Hija Hassan Hija (Kiwani) Jaku Hashim Ayoub (Muyuni) Rashindi Seif
(Ziwani0 Saleh Nassor Juma (Wawi) na Salim Abdalla Hamad (Mtambwe).
Wajumbe hao walitaka kujua
kwanini kumekuwepo na vitendo vya ubaguzi katika utoaji wa Vitambulisho
vya Mzanzibari Ukaazi kinyume cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984
pamoja na kila mwaka kutengwa fedha za matengenezo ya Ikulu bila ya
kuonekana mabadiliko yake.
Mawaziri waliosimama kuokoa
jahazi ni Waziri Nchi Fedha, Uchumi na Mipango, Omar Yussuf Mzee; Waziri
wa Afya, Juma Duni Haji; Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Mohamed Aboud Mohamed; Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa
Haji Gavu na Mwansheria Mkuu wa Serikali Othman Masoud Othman.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment