Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema ,John Mnyika |
Boniface Meena
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), kimelaani kukamatwa na
kushambuliwa kwa viongozi wa madaktari ikiwamo Dk Ulimboka Steven
ikieleza kuwa hatua hiyo haiwezi kuwa suluhu bali itachochea zaidi
mgogoro wa madaktari na Serikali.
Taarifa iliyotolewa jana na
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika inaeleza pia
kwamba udhaifu wa Serikali kuharakisha kwenda mahakamani kabla ya Bunge
kupewa fursa ya kujadili madai ya madaktari na kuisimamia Serikali
umelifikisha taifa katika hali iliyopo sasa.
"Nalaani uamuzi wa Serikali wa
kutumia vyombo vya dola kukamata na kushambulia viongozi wa madaktari
ikiwemo Dk Ulimboka Steven kwa hauwezi kuwa suluhu bali utachochea zaidi
mgogoro kati ya madaktari na Serikali," ilisisitiza sehemu ya taarifa
hiyo ya Mnyika na kuongeza:
“Nichukue fursa hii kuwaomba madaktari kufanya kila kinachowezekana kuokoa uhai wa wagonjwa katika kipindi hiki kigumu.”
Mnyika alisema kuwa ameomba
wabunge wapewe nakala ya Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii kuhusu
madai ya madaktari na hoja ya taarifa husika iwekwe katika orodha ya
shughuli za Bunge katika mkutano wa Bunge unaoendelea ili ijadiliwe na
kupitisha maazimio, kuwezesha hatua za muda mfupi, wa kati na muda mrefu
kuupatia ufumbuzi mgogoro huo na kuboresha sekta ya afya nchini.
“Natarajia
kwamba Spika atawezesha kamati kuwasilisha taarifa yake na Bunge
kujadili baada ya Serikali kutoa kauli yake bungeni,”alisema. Mnyika
alisema ikiwa wabunge wataelezwa ukweli na kupewa taarifa kamili
wataweza kuisimamia Serikali na kuwaeleza ukweli madaktari kipi
kinawezekana na kipi hakiwezekani.
Alisema kuwa ingawa Waziri Mkuu
Mizengo Pinda ametoa maelezo bungeni kuwa Serikali itatoa kauli bungeni
kuhusu mgomo huo, Bunge halitaruhusiwa kujadili kauli husika, hivyo
kukoseshwa fursa ya kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment