Tuesday, 24 April 2012
Pinda aziba masikio mawaziri kujiuzulu
Waandishi Wetu
WAKATI wabunge wakiendelea kusaini fomu ya majina ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni jana alikwepa kuzungumzia hatua za kinidhamu dhidi ya mawaziri wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali.Akiahirisha Mkutano wa Saba bungeni Dodoma, Pinda hakugusia suala la kujiuzulu kwa mawaziri wanane na badala yake alisema: “Siku zote Serikali imekuwa tayari kupokea ushauri wa Bunge baada ya kusikiliza mjadala na mapendekezo ya waheshimiwa wabunge.’’
Baada ya kuahirishwa kwa Bunge hadi Juni 12, mwaka huu. Pinda akiwa nje ya Bunge alikwepa kuzungumzia suala hilo licha ya kubanwa na waandishi wa habari na badala yake alicheka: "Haahaa," kisha akaingia kwenye gari na kuondoka.
Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema kitendo cha Pinda kushindwa kuzungumzia chochote kuhusu agizo la wabunge kutaka mawaziri wanane wawajibishwe, kimewaacha wananchi katika hofu.
Alisema Waziri Mkuu ametoa hotuba nyepesi kama vile taifa haliko katika giza kutokana na Bunge kutaka kuwajibishwa kwa mawaziri hao na kuapa kulifikisha suala hilo kwa wananchi.
“Aliahirisha shughuli za Bunge kama hakuna kitu kikubwa kilichohitaji majibu ya Serikali, wananchi walitaka kusikia mawaziri waliotajwa kwa tuhuma za ufisadi wakiwajibishwa lakini, hakuna chochote kilichofanyika. Sasa sisi tutakwenda kwa wananachi.
Jumamosi iliyopita, Pinda aliahidi kuwa jana Serikali ingeweka hadharani msimamo wake kuhusu suala baadhi ya mawaziri kutakiwa kujiuzulu lakini hakutekeleza ahadi yake.
Jana, Waziri Mkuu alisema Serikali itachukua hatua stahiki kuimarisha usimamizi na utendaji ndani ya wizara, Serikali za Mitaa na vyombo husika katika kuhakikisha watendaji wake wanafanya kazi kwa umakini.
Mawaziri wazidi kubanwa
Wakati Pinda akikwepa kuzungumzia suala hilo, joto la mawaziri kutakiwa kujiuzulu linazidi kupanda baada ya vigogo zaidi kuendelea kusaini fomu ya majina ya wabunge wasiokuwa na imani naye huku viongozi wa dini wakisema suala la mawaziri kung’oka ni la lazima.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa dini walisema kuwa suala la mawaziri hao kujiuzulu halina mjadala na kusisitiza kuwa kuwajibika kwa kiongozi kunamjengea heshima katika jamii.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini alisema kuwa kujiuzulu ni jambo la kawaida na kumtolea mfano Mzee Ali Hassan Mwinyi kwamba aliwahi kujiuzulu uwaziri na baadaye akachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania… “Kujiuzulu ni heshima siyo aibu… hili jambo mawaziri wote wanatakiwa kulitambua.”
Alisema kama ndani ya wizara imeibuka tuhuma na ikathibitishwa kinachofuata ni watendaji wakuu wa wizara husika kuachia ngazi.
Akizungumzia kitendo cha kupishana kwa kauli kati ya Waziri wa Viwanda na Biashara na wa Uchukuzi dhidi ya manaibu wao alisema, “Walitakiwa kuzungumzia tofauti zao katika vikao vya chama chao, siyo kujikosha katika vyombo vya habari.”
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum aliwataka mawaziri hao kuacha kujitetea katika mambo ambayo yanaonekana wazi kuwa yanawahusu.
“Hakuna sababu ya waziri kuanza kujiteteta katika jambo ambalo anaonekana wazi kuwa anahusika na ndiye mtendaji mkuu wa wizara yake,” alisema Sheikh Salum
Alisema mawaziri hao wanatakiwa kujiuzulu ili kulinda heshima zao huku akiwataka Watanzania kuwa na utaratibu wa kuwajibika pale wanapoona mambo hayako sawa.
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec), Askofu Yuda Thadei Ruaichi alisema: “Kama mtu umefanya mabaya kwa nini uendelee kung’ang’ania? Sisi tutakachokifanya ni kuwashauri watu kuhusu suala hili ila waondoke kama tuhuma zao zipo wazi.”
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Antony Lusekelo alisema taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaleza wazi hivyo hakuna haja ya mawaziri hao kusita kuwajibika.
Alisema mawaziri hao wanatakiwa kuwajibika kabla ya Watanzania kuamua kuingia mtaani na kufanya maandamano… “Wakati ule wa Richmond kuna ambao waliwajibika. Sasa hawa wanasita kufanya hivyo kwa misingi ipi? Ukimya wao unaipa wakati mgumu CCM.”
Kamati yamshukia Maige
Katika hatua nyingine Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imependekeza kuwajibishwa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kwa madai ya kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji.
Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, James Lembeli pia imependekeza Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Ladislaus Komba achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kutoa vibali vya kusafirisha wanyama hai kwenda Pakistan kinyume cha sheria.
Wakati akitoa vibali vya kusafirisha twiga wawili, viboko wawili na swala wanne kwenda Karachi, Pakistan mwaka 2010, Balozi Komba alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akisoma taarifa ya kamati hiyo bungeni jana, Lembeli alisema kamati yake pia inataka watumishi wote wa wizara hiyo waliohusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa hiyo nao washtakiwe.
Lembeli alisema ugawaji wa vitalu vya uwindaji ulitawaliwa na dosari nyingi ikiwamo waziri mwenye dhamana kutangaza majina ya waliopata vitalu bila kuonyesha ni vitalu vipi walipewa na kampuni zisizo na sifa kupewa vitalu hivyo.
Mwenyekiti huyo alisema kampuni tatu, Mwanauta and Company Ltd, Kawawa Hunting Safaris Ltd na Malagarasi Hunting Safaris ziligawiwa vitalu kinyume na mapendekezo ya kamati ya ushauri kwamba zisipewe vitalu kwa kuwa hazina sifa.
Katika tuhuma hizo, kamati hiyo imebainisha kuwa Waziri Maige ambaye pia ni Mbunge wa Msalala, Shinyanga azipatia vitalu kampuni 16 ambazo hazikuomba na vingi vya hivyo vikiwa ni vya madaraja ya kwanza na pili.
Lembeli alisema dosari hizo ziliathiri dhana ya uwazi na misingi ya utawala bora na kuashiria kuwapo kwa rushwa hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa kampuni nyingine zenye sifa ambazo zilinyimwa vitalu.
“Kamati inapendekeza Bunge liitake Serikali kumwajibisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Ezekiel Maige kwa kutengeneza mazingira ya rushwa ikiwa ni pomoja na kuyanyang’anya vitalu makampuni 16 yaliyogawiwa vitalu bila kuomba,” alisema Lembeli.
Mponda asubiri rungu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda alisema jana kwamba hatima yake ya kujiuzulu au kuendelea na uwaziri ipo kwa Waziri Mkuu.
Dk Mponda alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari juu ya taarifa za kuwa mmoja wa mawaziri wanaotakiwa kuachia ngazi. Alikuwa akizungumza nao kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Chanjo na Malaria Duniani.
Alisema amepokea taarifa hizo za kuwa mmoja wa mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu na lakini anasubiri uamuzi wa bosi wake.
Mkono asaini
Juzi usiku Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, juzi usiku alisaini fomu ya majina ya wabunge wasiokuwa na imani na Waziri Mkuu yanayokusanywa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto kabwe.
Zitto alikuwa akikusanya saini za wabunge wasiopungua 70 ambao ni asilimia 20 ya wabunge wote ili awasilishe hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa Spika wa Bunge.
Mkono alikuwa ni mbunge wa 74 na wa sita wa CCM kati ya 76 waliosaini fomu hiyo hadi jana mchana. Juzi usiku, Mkono alimpigia simu Zitto na kumtaka ampelekee fomu hiyo ili aweke saini yake.
“Mimi ni mjumbe wa NEC na nimepata nafasi hiyo kwa kuchaguliwa na wabunge wenzangu wa CCM, sasa ninapoona wabunge wenzangu wakiwemo wa CCM wanalalamikia utendaji wa mawaziri wetu kwa kuhusishwa na ufisadi wa fedha za umma na Serikali inakaa kimya ni lazima nichukue hatua,” alisema na kuongeza:
“Mawaziri wetu hata wafanye kosa gani sisi wabunge hatuwezi kuwawajibisha, ni mmoja tu naye ni Waziri Mkuu ambaye tunaweza kufanya hivyo. Sasa tumeona kuna mawaziri wamekutwa na kashfa mbalimbali na bado wanang’ang’ani kubaki kwenye nafasi zao hatuna jinsi, ili kuwang’oa nilazima tumuondoe Waziri Mkuu.”
“Sina tatizo na Pinda katika utendaji wake wa kazi lakini hatuwezi kuwaondoa mawaziri wenye kasoro bila ya kumwondoa yeye kwa mujibu wa sheria zetu, ndiyo maana nimesaini fomu hii kwa maslahi ya taifa langu.”
Wabunge CCM wanena
Baadhi ya wabunge wa CCM wametaka mchakato wa kuwang’oa mawaziri uende mpaka kwa watendaji wengine wa Serikali kwa kuwa ndiyo wahusika wakubwa wa matumizi mabaya ya fedha za umma.
Wabunge hao walitoa kauli hiyo jana katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Pia walipendekeza kutungwa kwa sheria itakayowajumuisha mawaziri na watendaji wakuu wa wizara na idara zinazotuhumiwa katika makosa ya uhalifu.
Mbunge wa Kalenga, Dk William Mgimwa alisema: “Hii siyo njia pekee ya kupambana na vitendo vya ubadhirifu serikalini lakini lazima tuanze na hatua hii ya kuwawajibisha mawaziri sababu ndiyo njia pekee ya kurejesha imani ya Serikali kwa wananchi.”
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina alitaka hadi kufikia kipindi cha Bunge kupitisha bajeti, watendaji wa Serikali wanaotumiwa na matumizi mabaya ya Serikali wawe wamechukuliwa hatua.
Alitaka makatibu wakuu wa Wizara na idara za Serikali, wakurugenzi wa miji na halmashauri za wilaya zinazotuhumiwa kwa ufisadi, kabla ya kikao cha Bunge la Bajeti la Juni, mwaka huu wawe wamechukuliwa hatua.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Geofrey Nyang’oro, Dar; Edwin Mjwahuzi, Masoud Masasi na Daniel Mjema, Dodoma
Source: Mwananchi Newspaper