MKULO ASEMA HAWAJIBIKI KAMATI KUU CCM, NUNDU ATOA MANENO MAKALI, MAIGE, "NIACHENI"
Rais Kikwete akifafanua jambo |
Ramadhan Semtawa na Boniface Meena
SIKU chache baada ya
Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kubariki uamuzi wa Rais
Jakaya Kikwete wa kulisuka upya Baraza la Mawaziri kwa kuwaondoa
waliotajwa katika Ripoti Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu wamekataa kuchukua hatua hiyo huku
mmoja wao, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo akisema hawajibiki kwa chombo
hicho cha chama.
Kwa wiki mbili sasa, kumekuwa na
shinikizo la kutaka mawaziri wanane wajiuzulu nyadhifa zao kutokana na
wizara zao kutajwa na CAG kwamba zimehusika na ufisadi huku wengine
wakitajwa moja kwa moja kufanya uamuzi wenye maslahi binafsi.
Wakizungumza na waandishi wetu
kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya mawaziri hao walisema wanaacha
hatima yao mikononi mwa Rais ambaye ndiye mamlaka ya uteuzi na kutengua
nafasi zao.
Mkulo
Mwandishi: Asalaam alaykum ndugu yangu Waziri Mkulo.
Mkulo: Walaykum Salaam.
Mwandishi: Habari ya mapumziko?
Mkulo: Aaah salama.
Mwandishi: Nimekupigia kutaka kujua msimamo wako kuhusu uamuzi wa CC.
Mkulo: Nakusikiliza endelea.
Mwandishi: CC imebariki Rais Kikwete afumue Baraza la Mawaziri ni kwa nini usijiuzulu kabla?
Mkulo: No comment, (sina la kusema).
Mwandishi: Lakini, CC ina nafasi kubwa katika utendaji wa Serikali, kwa nini huoni uzito wa agizo lake?
Mkulo: Mimi sijaona muhtasari wa vikao vya CC lakini, pia siwajibiki kwa CC.
Mwandishi: Kwa maana nyingine huwezi kujiuzulu?
Mkulo: No comment katika hilo.
Mkulo amekuwa akitajwa kutaka
kuvunja Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) kwa madai ya kuficha
kile kilichoitwa baadhi ya tuhuma za ufisadi katika uuzaji mali za umma
ikiwemo Kiwanja Namba 10 kilichopo Barabara ya Nyerere, kwa Kampuni ya
Mohamed Enterpises (MeTL).
No comments:
Post a Comment