MSANII
wa filamu, Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu, jana
alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku akibubujikwa
machozi kiasi cha kumfanya Hakimu Ritha Tarimo ambembeleze ili
kumnyamazisha.
Lulu anashtakiwa mahakamani hapo kwa kutuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba na alifikishwa jana kwa mara ya pili akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza na Polisi.
Lulu anashtakiwa mahakamani hapo kwa kutuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba na alifikishwa jana kwa mara ya pili akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza na Polisi.
Lulu alifikishwa mahakamani hapo
saa 3:06 asubuhi akiwa katika basi dogo la Magereza pamoja na mahabusu
wengine wanawake ambalo lilikuwa likisindikizwa na magari mengine mawili
na alikuwa chini ya ulinzi wa askari sita wa kike wa Magereza na askari
mmoja wa kike wa Polisi wakishirikiana na askari wa kiume wa Magereza
zaidi ya sita.
Mara baada kuingia katika chumba
cha Mahakama, Lulu ambaye alikuwa amevalia dira jekundu alianza kulia
kwa uchungu hali ambayo ilimlazimu Hakimu Tarimo pamoja na baadhi ya
askari kumnyamazisha.
Kutokana na
kujaa kwa watu mahakamani hapo, askari wa Kikosi Maalumu cha Magereza
walilazimika kuufunga mlango wa Mahakama hiyo ili kesi hiyo isikilizwe.
Baada ya kesi hiyo kutajwa,
Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda aliiomba Mahakama iamuru
watu wote watoke nje kwa sababu walikuwa wamefunga njia ili mtuhumiwa
huyo aweze kupitishwa.
Hakimu Tarimo alikubaliana na
ombi hilo na kuwaamuru askari kusafisha njia ili waweze kumpitisha
msanii huyo kwa kile alichosema kuwa Lulu bado ni mtuhumiwa na anaweza
kuumizwa.
“Askari safisheni njia ili mtuhumiwa aweze kupita kwa sababu yeye bado ni mtuhumiwa anaweza kuumizwa,"alisema Hakimu Tarimo.
Baada ya kutolewa kwa amri hiyo,
askari walitimiza wajibu wao na muda mfupi njia ilipatikana na msanii
huyo kutolewa mahakamani hapo.
Jopo la mawakili
Katika kesi hiyo, Lulu anatetewa
na jopo hilo la mawakili akiwemo Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu
na Utawala Bora (CHRAGG), Joaquine De- Melo, Kenedy Fungamtama, Peter
Kibatala na Fulgence Massawe.
De- Melo pia aliwahi kuwa Rais
wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) na mshindi wa Tuzo ya Mwanamke
Jasiri Tanzania ya Martin Luther King.
Fungamtama ambaye ndiye kiongozi
wa jopo la mawakili hao wanaomtetea Lulu, anakumbukwa kwa kuitetea
kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans, katika kesi dhidi ya
Tanesco, ambayo alishinda na shirika hilo kuamriwa kuilipa kampuni hiyo
zaidi ya Sh94 bilioni kwa kuvunja mkataba.
Kibatala ambaye pia anamtetea
kada wa Chadema, Fred Mpendazoe katika kesi ya uchaguzi Jimbo la
Segerea, pia ni Makamu wa Rais wa TLS, wakati Massawe anatoka Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Mawakili hao walijitokeza jana
mbele ya Hakimu Tarimo tayari kumtetea Lulu na baada ya mawakili hao
kujitambulisha, Wakili Kaganda alisema upelelezi wa kesi bado
haujakamilika na kuiomba Mahakama iipangie tarehe nyingine.
Hakimu Tarimo aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka huu itakapofikishwa mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa.
Kwa mara ya kwanza Lulu
alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi,
Augustina Mmbando akikabiliwa na la shtaka hilo la mauaji.
Wakili Kaganda alimsomea hati ya
mashtaka alidai kuwa Aprili 7, mwaka huu katika maeneo ya Sinza
Vatican, Wilaya ya Kinondoni, mtuhumiwa alimuua Kanumba. Kanumba
alifariki dunia siku hiyo saa 9:00 usiku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni
baada ya ugomvi baina yake na Lulu.