MOTO uliowashwa bungeni na wabunge kuibana serikali baada ya
kuwasilishwa kwa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG),
sasa umewalazimu mawaziri wanane kutakiwa kupima uzito wa makosa yao na
kufanya maamuzi ikiwa ni pamoja na kutakiwa kung’oka.
Alhamisi usiku, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alitoa wito kwa
wabunge wote kujiorodhesha kwa nia ya kupata saini za wabunge 71 ambao
wangewasilisha kutimiza matakwa ya kisheria kupata asilimia 20 ya
wabunge kwa ajili ya kumuondoa Waziri Mkuu.
Mawaziri ambao usiku huu tayari wamejipinda kumuandikia barua Rais
Jakaya Kikwete, kwa ushauri wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuikoa serikali
ya chama hicho isianguke kutokana na mpango wa wabunge kujirodhesha
kutaka kumuondoa Waziri Mkuu,Mizengo Pinda.
Wanaotakiwa kuondoka ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa
Viwanda na Biashara, Cyril Chami, Waziri wa Nishati na Madini, William
Ngeleja, Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, Waziri wa Maliasili na Utalii,
Ezekiel Maige, Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi),George Mkuchika, Waziri wa Kilimo Chakula
na Ushurika Jumanne Maghembe na Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda.
Hata hivyo, baadhi ya Mawaziri hao, wameelezea kuwa wataandika barua
kwa Rais Kikwete kuelezea uozo wote uliosababisha kusakamwa kwao, baadhi
wakidai kwamba hawahusiki kwa lolote na mambo wanayotuhumiwa nayo, huku
baadhi wakiona mambo ni mazito na kuamua kujiondoa usiku huu.
Chanzo - Fikra Pevu