Sunday, 18 March 2012

GAZETI LA MWANANCHI: Dk Mwakyembe arejea, kutoa neno Jumatatu


Dk Mwakyembe
NA Fidelis Butahe
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe amerejea nchini akitokea India alikokwenda kwa matibabu na kueleza kuwa atazungumzia, pamoja na mambo mengine, afya yake kesho atakapoingia ofisini.

Hata hivyo, mara baada ya kuwasili jana alasiri kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam Mbunge huyo wa Kyela (CCM), hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari na badala yake alitoa ujumbe wake huo kupitia kwa Mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa ambaye pia ni msemaji wa familia ya Dk Mwakyembe.

Mwambalaswa alisema Dk Mwakyembe aliona ni vyema apate muda wa kutosha kujiandaa kabla ya kukutana na waandishi wa habari Jumatatu.

“Afya yake imeimarika na anaendelea vizuri, ila ameomba msamaha kuwa hataweza kuzungumza na nyinyi (waandishi), amesema yeyote anayetaka kuzungumza naye, aende ofisini kwake Jumatatu,” alisema Mwambalaswa.

Dk Mwakyembe alifika katika viwanja hivyo saa 9:47 alasiri, lakini kabla ya kuingia katika vyumba vya abiria wanaowasili, alituma ujumbe kwa waandishi wa habari kuwa hatakuwa tayari kuzungumza jambo lolote.
Dk Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo Oktoba 9, mwaka jana yalimlazimu kupelekwa katika Hospitali ya Appolo, India kwa matibabu zaidi.

Maradhi hayo yamezua utata mkubwa baada ya kudaiwa kuwa yametokana na kuwekewa sumu huku kukiwa na kauli mbalimbali zinazotofautiana kutoka kwake na baadhi ya watendaji wengine wa Serikali.

Kauli tata zaidi ziliibuka baada baadhi ya viongozi akiwamo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta kudai kuwa maradhi yanayomsumbua Dk Mwakyembe yametokana na kulishwa sumu.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba alijibu madai hayo aliposema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa Dk Mwakyembe hajaugua kwa sababu ya kulishwa sumu na kutishia kuwachukulia hatua walitoa kauli hizo.

Ripoti ya uchunguzi aliyoisoma Manumba katika mkutano wake na waandishi wa habari Februari 16, mwaka huu Dar es Salaam, inaonyesha kuwa Dk Mwakyembe hakulishwa sumu huku akisema kwamba pia ulijumuisha taarifa kutoka hospitalini India ambako alikuwa anatibiwa.

Alisema uchunguzi huo unalipa Jeshi la Polisi picha kuwa waliotoa taarifa hizo hadharani wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Baada ya kauli hiyo, Dk Mwakyembe aliibuka na kutoa kauli nzito iliyoonekana kumjibu Kamishna Manumba akielezea kushangazwa kwake na majibu hayo huku akisisitiza kuwa madaktari waliokuwa wakimtibu walithibitisha kuwa ugonjwa alionao unatokana na kulishwa sumu.

Mbali ya Dk Mwakyembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, kwa nyakati tofauti walikana kuijua ripoti hiyo ya Kamishna Manumba.

Hata hivyo, katika kile kilichoonekana kudhamiria kuchukua hatua, inadaiwa kuwa Kamishna Manumba aliwasilisha jalada la mashtaka kwa watu hao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi ambaye alithibitisha kulipokea lakini akasema ni vigumu kufahamu ni lini atakapopeleka mahakamani jalada la kesi kwa watu hao.

“Ni vigumu kusema ni lini kesi itapelekwa mahakamani... bado tunalifanyia kazi,” alisema Feleshi akisisitiza kuwa uamuzi wa kupeleka suala hilo mahakamani utategemea uchunguzi unaofanywa na ofisi yake.

No comments:

Post a Comment