Tuesday 21 February 2012

UTATA GANI KATIKA AFYA YA DK. MWAKYEMBE?

NI NINI hasa kinachomsibu Dk. Harrison Mwakyembe? Je, kuna ukweli kuhusu "kulishwa sumu" kama ilivyonenwa na Sitta? Bado utata utata unaghubika suala hili, hivi, ni serikali haitaki kuzungumzia suala hili? Ni wazi kabisa kwamba uchunguzi wa madaktari upo wazi kabisa, sasa utata unapokuja kwanini kutupiana mpira juu ya nani azungumzie suala hilo ndicho kitu pekee kinaleta wasiwasi mkubwa kwamba kuna siri nzito juu ya afya yake.


Itakumbukwa kwamba, Desemba 10 mwaka jana, Dk Mwakyembe akiwa na hali mbaya alipelekwa katika Hospitali ya Appolo, nchini India kwa matibabu baada ya kuugua maradhi yaliyosababisha ngozi yake kuharibika. Tangu arejee mwanzoni mwa mwezi uliopita alikuwa hajaonekana hadharani, mbali na kutoa tamko kwamba afya yake ilikuwa inaendelea vizuri.

Hata hivyo, muda wote huo aliokuwa nchini India na baada ya kurudi nchini, mazungumzo ya watu maofisini, nyumbani, mitaani na vijiweni yalitawaliwa na utata wa suala la afya ya Dk Mwakyembe, huku uvumi, tetesi na minong’ono kwamba maradhi yake yalisababishwa na hujuma za kisiasa vikitawala hisia za wananchi. Hisia hizo zilikuzwa na kauli ya mmoja wa washirika wake kisiasa, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta ambaye alimtembelea hospitalini nchini India na baadaye kukiambia kituo kimoja cha televisheni hapa nchini kwamba Dk Mwakyembe alikuwa amelishwa sumu kutokana na msimamo wake dhidi ya mafisadi.

Akizungumza huku akionyesha kujiamini, Waziri Sitta alisema muda wote aliokaa na naibu waziri huyo katika Hospitali ya Appolo alipata ushahidi wa kutosha kwamba maradhi yake ya kuharibika kwa ngozi ya mwili wake yalisababishwa na kulishwa sumu, huku ushuhuda wake ukiacha kitendawili cha nani hasa waliohusika na uhalifu huo pasipo kuteguliwa. Hata hivyo, kauli hiyo ya Waziri Sitta iliwaudhi viongozi wengi serikalini na katika chama chake cha CCM ambao walimtaka athibitishe tuhuma kwamba hujuma kwa Dk Mwakyembe ilikuwa ni kazi ya mafisadi.

Lakini jambo la kushangaza ni kwamba muda wote huo Serikali ilikataa kutoa tamko siyo tu kuhusu maradhi yanayomsumbua kiongozi huyo, bali pia kama ilikuwa imefanya upelelezi kuhusu kuwapo au kutokuwapo watuhumiwa wowote ambao walikuwa wanahusishwa na hujuma hiyo. Wananchi walishangazwa na hatua ya Serikali kuendelea kukaa kimya na kupiga danadana suala hilo, huku viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Afya wakitupiana mpira.

Tunashangazwa na ukimya huu wa Serikali hata baada ya kupata ripoti ya madaktari wa Hospitali ya Appolo ambao walimtibu Dk Mwakyembe. Haki ya wananchi kujua maradhi yanayomsibu inapewa uzito na ukweli kwamba yeye siyo tu mbunge wa kuchaguliwa na wananchi, bali pia ni naibu waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne. Tukitilia maanani kwamba gharama kubwa za matibabu yake zimelipwa kwa kodi za wananchi, ndipo tunaposhangaa kwa nini Serikali haioni uhalali wa wananchi kujua hali ya afya za viongozi wao kwa madai kwamba masuala ya afya zao ni masuala binafsi.

Alipojitokeza hadharani mwishoni mwa wiki akiwa na washirika wake wa kisiasa katika uzinduzi wa programu ya moja ya madhehebu ya Kikristo jijini Dar es Salaam, Dk Mwakyembe aliwaeleza waumini jinsi maradhi yake ilikuwa kazi ya mafisadi ambao walimsababishia mateso makubwa na kuahidi kuzungumzia suala hilo kwa undani katika siku za usoni, huku Waziri Samwel Sitta akisimama na kuwaeleza waumini kwamba Dk Mwakyembe alilishwa sumu.

Sisi tunadhani ukimya huu wa Serikali umeiletea aibu kubwa na kuibua hisia kwamba, pengine nayo ni sehemu ya tatizo. Vinginevyo haiingii akilini jinsi Serikali siyo tu inavyoweza kupata ujasiri wa kuficha ripoti iliyotolewa na Hospitali ya Appolo, bali pia kushindwa angalao kutoa tamko kama Dk Mwakyembe alilishwa sumu au la.

Kwa kuwa Dk Mwakyembe anajua fika nini kilichomo katika ripoti iliyotolewa na hospitali hiyo ya nchini India, tunamshauri ajitokeze hadharani awaeleze wananchi ukweli kwa lengo la kumaliza uvumi, tetesi na minong’ono kuhusu maradhi yanayomsibu.

No comments:

Post a Comment