Saturday 14 July 2012

Viongozi wa Chadema Walipokwenda Kituo kikuu cha Polisi DSM kuhojiwa

Siku ya Ijumaa, Julai 13, 2012 majira ya saa 4:27 asubuhi gari lenye namba za usajili T 875 AKS aina ya Toyota Landcruiser, liliwasili katika maegesho ya wizara ya mambo ya ndani na kisha akashuka Godbles Lema, Dkt. Willibrod Slaa pamoja na wakili wao Dkt. Rugemereza Nshala, kwa pamoja wakawa wanaelekea mlango wa kuingilia ndani ya jengo hilo.


Kabla ya kuingia ndani waandishi walitaka kujua sababu za Dkt. Slaa pamoja na Lema kufika makao makuu ya jeshi la polisi ambapo walisema walienda kuitikia wito.

“Tumepata wito na tumeitikia tambueni mjumbe hauawi sasa ni wito wa namna gani ngoja tukawasikilize lakini na ninyi waandishi wa habari hampitwi na kitu kila sehemu mpo,” alisema Dkt. Slaa huku akicheka.

Baada ya kufika mapokezi, Dkt. Slaa na Lema walielekezwa kwenda chumba namba 703 ambapo walikaa kwa muda wa dakika tano na kisha wakatoka kuelekea chumba namba 808 huku ofisa wa Polisi aliyevaa kiraia akiwataka waandishi wa habari wasiwafuate.

Katika Chumba namba 808 walichoingia ofisa huyo wa Polisi aliwakaribisha huku akisikia kuwaambia Dkt. Slaa, Lema pamoja na wakili wao Dkt. Nshala kuwa wakaribie ingawa eneo hilo lipo katika ukarabati na kisha kufunga mlango.

Akiongea na waandishi wa habari, msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema Dkt. Slaa na wenzake waliitwa kwa ajili ya maelezo ya awali ya kusaidia uchunguzi dhidi ya malalamiko yao ya kuuawa.

Alisema Jeshi la Polisi limefungua jalada la uchunguzi na kwamba mlalamikaji ni ni lazima atoe maelezo yatakayoweza kufanyika kwa uchunguzi huo kabala ya jalada kupelekwa kwa Mwendesha Mashitaka, “Tumewaita kwa hati maalum, dhidi ya malalamiko yao. Naamini tutashirikiana nao kubaini ukweli na kisha tutafanyia kazi kwa kuwa wajibu wetu ni kumlinda kila mmoja hata kama atakuwa ametolea malalamiko yake chumbani.” alisema Senso.


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka, Dkt. Slaa alisema suala aliloitiwa ni juu ya malalamiko yao ya kutishiwa kudhuriwa. Akasema alichowaeleza ni kwamba wanapaswa kuyatolea kwanza maelezo, taarifa za nyuma za kutishiwa kwao ikiwamo suala zima la kuwekewa vinasa sauti wakati akiwa mbunge mjini Dodoma, “Kila kitu kipo wazi nimewaambia kwa sasa sina maelezo mengine zaidi ya yale niliyotoa katika mkutano na waandishi wa habari, na kubwa nikawataka wanipe mrejesho wa taarifa mbali mbali za kutishiwa kwetu tulizowafikishia kabla” alisema Dkt. Slaa.

Wakili aliyefuatana na viongozi hao Dkt. Rugemereza Nshala, alisema wateja wake wameahidi kupeleka maelezo waliyotoa mbele ya waandishi wa habari na kwamba suala la kuhojiwa ni la kisheria hivyo wananchi wasubiri kujua kitu gani kitaendelea, “Jumatatu tutaleta yale yaliyoongelewa mbele ya waandishi wa habari na wao wafanyie kazi kuanzia hapo kuhusu kuhojiwa kwa wateja wangu hapa wamekuja kuitikia wito halali hivyo tusubiri nini kitafuata” alisema Dkt. Nshala.

Jumapili ya wiki iliyopita Dkt. Slaa akiwa na viongozi wengine wakuu wa CHADEMA walisema wamebaini mkakati wa makusudi wa kuwadhuru viongozi wakuu wa chama hicho, mpango waliosema unaratibiwa na baadhi ya vigogo katika Idara ya Usalama wa Taifa.


No comments:

Post a Comment