Friday 22 June 2012

Ikulu: Mashangingi sasa basi:::Gazeti la Mwananchi



Boniface Meena na Fidelis Butahe
OFISI ya Rais, Ikulu imesema Serikali itaanza kuwakopesha viongozi wake wa ngazi mbalimbali magari madogo ya gharama nafuu ili waachane na mashangingi yanayotumika sasa.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliliambia gazeti hili kuwa mpango huo unaotarajiwa kuanza Julai mwaka huu, una lengo la kupunguza matumizi ya Serikali kwa kuondokana na magari makubwa yenye gharama kubwa za uendeshaji.

Balozi Sefue alisema mpango huo unaanza katika mwaka huu wa fedha ambapo yatachambuliwa magari yanayofaa na yatapendekezwa yatumike katika shughuli gani.

Alipoulizwa kama mabadiliko hayo yatawagusa mawaziri na majaji, Balozi Sefue alisita kulijibu hilo na badala yake alisema kuwa bado suala hilo lipo katika mjadala.

“Hili jambo bado linajadiliwa, haya yote yatafanyika katika mwaka huu wa fedha,” alisema Balozi Sefue. Mwaka wa fedha unaaza Julai mosi mwaka huu.

Akifafanua zaidi alisema, “Kwanza tutatizama gari husika linatumia mafuta kwa kiwango gani, pia tutatizama hata gharama nyingine kama ufundi,” alisema Balozi Sefue.

Alisema kuwa utaratibu huo ukianza viongozi wanaotumia magari ya Serikali wataanza kukopeshwa magari hayo na kupewa posho kwa ajili ya kuweka mafuta.

“Ni kipaumbele cha Serikali kuangalia hilo mwaka huu na hata katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13 imeelezwa wazi, lengo ni kupunguza gharama za uendeshaji,” alisema Sefue.

Aliongeza, “Badala ya kumpa mtu gari tunamkopesha halafu tunakuwa tunampa mafuta ili kupunguza matumizi Serikalini.”

Alisema katika uchambuzi huo wataangalia ni kiongozi gani atahitaji gari la Serikali na yupi atatakiwa kukopeshwa na kwamba hali hiyo itafuatana na kazi za mtumishi husika.

“Tunaangalia hili la magari, lengo ni kuwa na magari ya aina fulani lakini si ya kifahari na tutawakopesha  watumishi,” alisema Sefue.

Alisema kuwa katika uchambuzi huo pia watazingatia ubora wa gari husika ikiwa ni pamoja na kustahimili kusafiri masafa marefu, kulingana na majukumu ya mtumishi.

“Yapo mambo ambayo Serikali imeyapanga na lazima yatekelezwe,” alisema Sefue.

Alipoulizwa kama mpango huo ni utekelezwaji wa mpango uliotolewa na Wizara ya Ujenzi mwaka 2004 wa kubana matumizi ya magari ya Serikali alisema hilo linaweza kutolewa ufafanuzi na Wizara ya Ujenzi yenyewe.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Herbert Mrango alipoulizwa kuhusu utekelezaji wa mpango huo alisema hawezi kuzungumzia mambo ya Serikali kwenye simu.

Wakati Balozi Sefue akisema hayo tayari kuna baadhi ya viongozi Serikalini wameshajikopesha magari hayo akiwemo Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu.

Suala la Ndulu kujikopesha gari lilielezwa hivi karibuni na Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe alipokuwa akisoma bajeti mbadala ya kambi rasmi ya upinzani bungeni.

Zitto alisema Serikali inatakiwa kupunguza mzigo wa matumizi ya magari ya Serikali kwa kupiga mnada baadhi ya ‘mashangingi’ na kuweka mfumo wa kukopesha magari kwa watumishi wote wa umma wanaostahili magari kama alivyofanya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

Balozi Sefue alipoulizwa kuhusu suala la Ndulu kujikopesha gari alisema hajuI bali huo unaweza ukawa ni utaratibu wa Bodi ya Wakurugenzi ya BoT ndiyo ambayo inaweza ikawa imepitisha hilo.
“Kwa maana ya framework hakuna kinachomzuia kufanya hivyo,” alisema.

Katika mkutano wa 7 wa Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), John Cheyo alieleza kuwa kumekuwa na matumizi yasiyo ya lazima katika uendeshaji na ukarabati wa magari hayo na hadi Juni 30, 2010 Serikali ilikuwa inamiliki magari yenye thamani ya Sh5 trilioni.
Alisema mwendelezo wa ununuzi wa magari unaofanywa na Serikali unaongeza gharama za uendeshaji na kusisitiza kwamba matumizi hayo si ya lazima kwa Serikali yenye uchumi mdogo uliozidiwa na madeni.

No comments:

Post a Comment