Wednesday 8 February 2012

"Aliyefufuka" Afrika Kusini ni tapeli

Mtu aliyedai kuwa ni mwanamuziki mashuhuri aliyekufa na kufufuka Afrika Kusini ameshtakiwa kwa udanganyifu, polisi wamesema.
Mtu huyo alisema yeye ni Khulekani "Mgqumeni" Khumalo - mwanamuziki maarufu wa miondoko ya Kizulu ambaye alifariki mwaka 2009. Amedai kuwa alitekwa nyara na mchawi ambaye alimfanyia mazingara na kumfungia katika pango na mizuka wengine, vimeripoti vyombo vya habari vya Afrika Kusini.
Lakini polisi wamesema alama za vidole vya mtu huyo vimeonesha sio mwanamuziki anayedai kuwa, bali jina lake halisi ni Sibusiso John Gcabashe, mwenye umri wa miaka 28.
"Kufufuka" kwa Khumalo kulizua tafrani na mashabiki wake kumiminika nyumbani kwake mwishoni mwa wiki, kiasi cha polisi wa kutuliza ghasia kuitwa na kutumia maji yenye nguvu kudhibiti umati wa watu.
Mtu huyo aliyejidai "amefufuka" amefikishwa katika mahakama ya mwanzo ya Nquthu iliyopo Kwazulu-Natal siku ya Jumanne ambapo ameshtakiwa kwa kosa la udanganyifu. Hakutakiwa kujibu lolote, amesema msemaji wa polisi Kanali Jay Naicker.
Amesalia rumande hadi Februari 14 ambapo ataruhusiwa kuomba dhamana na pia kusikia kama anakiri au kukana mashtaka yake.
Familia ya marehemu Khumalo ilionekana kugawanyika kuhusiana hasa na utambulisho kamili wa mtu huyo, huku wake zake wawili wakisema ni yeye, lakini rafiki wa zamani wa kike wa mwanamuziki huyo, Zehlise Xulu, akisisitiza kuwa sio mwenyewe.
Bi Xulu ambaye alizaa naye mtoto wa kiume ambaye ana umri wa miaka 10 sasa, amesema ana matumaini kuwa mtu huyo atakutwa na hatia na kufungwa jela kwa miaka mingi kutokana na "kurejesha majonzi ya zamani".
"Mwanangu alisafiri hadi Johannesburg akiwa na matumaini ya kumuona baba yake, badala yake alikuta mtu mwenyewe ni mhuni tu," amesema Bi Xulu akikaririwa na gazeti la Mercury.
"Nilikasirishwa sana kila mara alipokuwa akiniita mpenzi wake," amesema.
Imani za uchawi ni jambo la kawaida Afrika Kusini, hasa maeneo ya vijijini.
~BBC

No comments:

Post a Comment