Thursday 5 July 2012

Bajeti ya Ikulu Z’bar chupuchupu kukwama

Na Mwinyi Sadallah Zanzibar 


Bajeti ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais (Ikulu) Zanzibar imepita kwa mbinde, baada ya vifungu vingi vya matumizi ya fedha kukosa maelezo ya kina na kulazimika wajumbe kuzuia matumizi ya Sh. milioni 190 katika bajeti hiyo.

Hali hiyo imejitokeza wakati Baraza la Wawalikishi (BLW) lilipokaa kama kamati ya matumizi kupitisha vifungu vya bajeti hiyo chini ya Mwenyekiti wake Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho.

Fedha zilizozuiwa na wajumbe ni Sh. milioni 50 ambazo zilikuwa zitumike kununua televisheni kwa matumizi ya Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Sh. milioni 150 ambazo zilikuwa zitumike katika mradi wa kilimo wa ushirikiano kati ya serikali ya Zanzibar na Misri mwaka huu.

Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa Ladhu, alisema kwamba haiwezekani Sh. milioni 40 kutumika kwa manunuzi ya seti za televisheni wakati huduma nyingi zinakabiliwa na matatizo na kutaka fedha hizo zisipitishwe.

Hata hivyo Waziri mwenye dhamana wa Wizara hiyo, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, alisema kwamba wakati wa kutayalisha bajeti hiyo walikosea fedha hiyo imekusudiwa kununua jenereta na siyo televisheni.

Kutokana na utata huo Baraza liliamua kutopitisha kifungu hicho cha matumizi na kuwataka watendaji wakuu wa serikali kuwa makini wanapotayarisha bajeti za serikali.

Aidha, wajumbe hao pia wamesitisha matumizi ya Sh. milioni 150 ya utekelezaji wa mradi wa kilimo cha mbogamboga wa ushirikiano kati ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Misri.


Mwakilishi wa Jimbo la Mkwajuni Mbarouk (CCM), Wadi Mussa, alisema kwamba tangu mradi huo ulipoazishwa SMZ imekuwa hainufaiki na tayari Sh. bilioni moja zimetumika katika uendelezaji wa mradi huo.

Alisema hakubaliani na kuidhinishwa kwa Sh. milioni 300 wakati mazao yanayozalishwa katika shamba hilo yamekuwa yakivunwa na kusafirishwa kwenda Misri bila ya Zanzibar kunufaika na mradi huo.

Akishagiliwa na wajumbe alisema kwamba Kamati ya Fedha na Uchumi ilipotembelea mradi huo imegundua hata mkataba wake hauna tija kwa Zanzibar na umelenga kuipatia shamba la kilimo serikali ya Misri visiwani humo.

Hata hivyo Waziri Mwinyihaji, alisema kwamba mradi huo lengo lake kubwa ni kufanya utafiti wa mbengu za mazao tofauti na jina linalotumika katika mkataba wa mradi, jambo ambalo lilipingwa na wajumbe wa baraza hilo.

Mwakilishi huyo alisema kwamba kazi za utafiti wa mbegu na mazao zinatakiwa kufanywa na wanasayansi wakiwemo wataalamu wa kilimo na siyo askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi ambao wamepewa kazi ya utekelezaji wa mradi huo.

Kutokana na utata wa maelezo ya Waziri, wajumbe wa baraza hilo kwa kauli moja waliamua fedha hizo kusitishwa matumizi yake hadi tathimini ya mradi huo itakapofanyika kuangalia faida na hasara yake.

Maeneo mengine yaliyotaka kuikwamisha bajeti hiyo ni matumizi ya Sh. milioni 110 yaliyopangwa kutumika katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya viburudisho katika Idara ya Utumishi na Uendeshaji kutoka Sh. milioni 6 katika bajeti ya mwaka jana.

Aidha, Jussa alitaka kujua kwa nini bajeti hiyo imejaa vifungu vya matumizi ya fedha na kupewa jina la posho maalum huku kukiwa hakuna maelezo juu ya watu watakaonufaika na posho hilo.

Jussa, pia alipinga matumizi ya Sh. milioni Sh. 337.5 fedha ambazo zimependekezwa kutumika kama ada ya mikataba katika idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari mkazi katika mwaka huu wa fedha.

Wajumbe wengine waliyozuia vifungu vya bajeti hiyo ya Ikulu, ni Asha Bakari Makame, (Viti Maalum) Hija Hassan Hija (Kiwani) Jaku Hashim Ayoub (Muyuni) Rashindi Seif (Ziwani0 Saleh Nassor Juma (Wawi) na Salim Abdalla Hamad (Mtambwe).

Wajumbe hao walitaka kujua kwanini kumekuwepo na vitendo vya ubaguzi katika utoaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari Ukaazi kinyume cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na kila mwaka kutengwa fedha za matengenezo ya Ikulu bila ya kuonekana mabadiliko yake.

Mawaziri waliosimama kuokoa jahazi ni Waziri Nchi Fedha, Uchumi na Mipango, Omar Yussuf Mzee; Waziri wa Afya, Juma Duni Haji; Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed; Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Gavu na Mwansheria Mkuu wa Serikali Othman Masoud Othman.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment