Sunday, 22 April 2012

MGAO WA MALI ZA MAREHEMU STEVEN KANUMBA WALETA MGOGORO KWENYE FAMILIA

 
(Mama wa marehemu Steven Kanumba, Bi. Flora Mutegoa.)

Habari na Gazeti la Mwananchi

Wiki mbili baada ya kifo cha aliyekuwa msanii nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba, wazazi wake; Charles Musekwa Kanumba na Mama yake, Flora Mutegoa ambao hawaishi pamoja, wametofautiana kuhusu suala la mali na mirathi.

Juzi, Mzee Kanumba aliibuka na kudai kuwa kuna kundi la watu linalomdanganya mama huyo wa marehemu kwamba linajua zilipo mali za Steven jambo ambalo alisema ni uongo na kumtaka awe na subira na asidanganyike.

Hata hivyo, kauli hiyo imepingwa na Mutegoa ambaye amehoji sababu za mumewe huyo kuzungumzia mali za mwanaye wakati huu. Alidai kuwa Mzee Kanumba hajawahi kuwa na mawasiliano na marehemu tangu mwaka 1999 alipoondoka kwao, Shinyanga.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili juzi, Mzee Kanumba alimsihi mkewe kutodanganyika kwa kuwa yeye akiwa baba mzazi wa Kanumba anajua mali zote za mtoto wake na ndiye pekee anayeweza kumtendea haki katika kuzigawa.

“Mali za marehemu mwanangu nazifahamu zote, kwa hiyo hakuna shaka tutazigawa kwa sababu hakuna baba mwingine na haki yangu ipo palepale hakuna atakayeinyang’anya,” alisema na kuongeza:

“Nisingependa tuwape watu faida ya kuanza kuvutana mahakamani, tunatakiwa suala hili tulimalize sisi wenyewe kama tulivyompata mtoto wetu. Ninasisitiza mali zote zisifanyiwe vurugu ziachwe kama zilivyo.”
Katika kuthibitisha kwamba anazijua mali hizo, mzee huyo alisema Steven ameacha magari matatu, Sh40 milioni, viwanja viwili na akaunti mbili za benki na Kampuni ya Filamu.

Akerwa na tambiko
Mzee Kanumba alisema anasikitishwa na tambiko la Kihaya lililofanyika katika kaburi la mtoto wake, jambo ambalo alisema halikutakiwa kwa kuwa marehemu alikuwa Mkristo na alizikwa kwa imani hiyo.

“Mimi ni Mkristo, mtu aliyezikwa Kikristo huwezi tena kuanza kumfanyia mambo ya kipagani na kuanza kumtambikia, hiyo kwetu hairuhusiwi,” alisema Mzee Kanumba na kuongeza:

“Hata hivyo, marehemu alikuwa Msukuma, si Mhaya, itakuwaje wamtambikie Kihaya na kumwaga pombe aina ya rubisi huku marehemu alikuwa hatumii pombe na mimi pia situmii pombe?”

Kuhusu tambiko, Flora alisema hakuna kitu kama hicho kilichofanyika kwenye kaburi la mwanaye isipokuwa Wahaya wana mila zao kwa mwenzao aliyepatwa na msiba.

“Kilichofanyika siyo tambiko bali, ni mila zetu za Kihaya. Unapofiwa wenzako wanakuletea vitu kama kreti ya soda, bia na mkungu wa ndizi. Lile siyo tambiko ni mila tu, mimi pia ni Mkristo, siwezi kushiriki matambiko,” alisema.

Alisema suala hilo la kugawa mali au msimamizi wa mirathi walitakiwa kukutana pande mbili, yaani yeye na mkewe baada ya kupita siku 20 tangu alipozikwa waangalie namna ya kugawa huku akisisitiza kuwa hakuna mtu mwingine anayeruhusiwa kuingilia masuala hayo.

Mama amkana
Kwa upande wake, Mutegoa ambaye sasa bado yupo nyumbani kwa Kanumba, Sinza Vatican, Dar es Salaam alisisitiza kwamba marehemu hajawahi kuwasiliana na baba yake huyo tangu mwaka 1999.

Alieleza kushangazwa na taarifa hizo kutoka kwa mzazi mwenzake huyo na kusisitiza kuwa ni mapema mno kuanza kujadili mali za mtoto.

“Nasikitika kulisema hili kwani bado niko kwenye msiba wa mwanangu. Hata hivyo, sidhani kama mwenzangu anajua chochote kuhusu Steven, achilia mbali mali zake, hawajawahi kuwa na ukaribu mpaka kuweza kujua mali zake,” alisema na kuongeza:

“Hata hivyo, mbona anazungumzia mali tu, hivi anafahamu kama Steven alikuwa na madeni? Ninamsihi aachane na hizo habari kwa wakati huu kwani hazina uzito wowote ukilinganisha na thamani ya mtoto niliyempoteza,” alisema.