Saturday 21 April 2012

Mawaziri Wanane watakiwa kung'oka wamuandikia Barua Kikwete

MOTO uliowashwa bungeni na wabunge kuibana serikali baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), sasa umewalazimu mawaziri wanane kutakiwa kupima uzito wa makosa yao na kufanya maamuzi ikiwa ni pamoja na kutakiwa kung’oka. 
Alhamisi usiku, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alitoa wito kwa wabunge wote kujiorodhesha kwa nia ya kupata saini za wabunge 71 ambao wangewasilisha kutimiza matakwa ya kisheria kupata asilimia 20 ya wabunge kwa ajili ya kumuondoa Waziri Mkuu. 
 Mawaziri ambao usiku huu tayari wamejipinda kumuandikia barua Rais Jakaya Kikwete, kwa ushauri wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuikoa serikali ya chama hicho isianguke kutokana na mpango wa wabunge kujirodhesha kutaka kumuondoa Waziri Mkuu,Mizengo Pinda.
Wanaotakiwa kuondoka ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),George Mkuchika, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushurika Jumanne Maghembe na Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda. 
 Hata hivyo, baadhi ya Mawaziri hao, wameelezea kuwa wataandika barua kwa Rais Kikwete kuelezea uozo wote uliosababisha kusakamwa kwao, baadhi wakidai kwamba hawahusiki kwa lolote na mambo wanayotuhumiwa nayo, huku baadhi wakiona mambo ni mazito na kuamua kujiondoa usiku huu. Chanzo - Fikra Pevu