Thursday 12 July 2012

Mdee arusha kombora


Mh. Halima Mdee
KAMBI ya upinzani bungeni imeitaka serikali kuyarejesha mashamba yaliyoshindwa kuendelezwa na wawekezaji na yagawiwe kwa wananchi wenye kuyahitaji.

Miongoni mwa wawekezaji hao ni Chavda Group, aliyeuziwa mashamba saba yenye ukubwa wa hekta 25,000, katika maeneo tofauti hapa nchini, ambapo mwaka 1993 alizitumia hati zake kujipatia mkopo wa dola milioni tatu.

Kauli hiyo imetolewa jana bungeni na Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, alipokuwa akitoa hotuba ya kambi yake kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2012/2013.

Mdee alisema familia ya Chavda iliahidi kufufua mashamba ya mkonge Tanga ndani ya miaka 10, na kupata dola milioni 42 lakini walipopata fedha hizo hawakufanya lolote kwenye mashamba hayo na hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yao.

”Tuwachukulie wawekezaji wa aina hii kama ni ’waporaji’ na hawana tofauti na majambazi wanaoiba benki kwa kutumia nguvu,” alisema Mdee.

Aliongeza kuwa wanaitaka serikali kuyarejesha serikalini bure pasi na fidia mashamba hayo kwa ajili ya kutafuta wawekezaji wengine wenye mtaji wa kutosha watakaoyaendeleza.

Alibainisha kuwa mashamba ambayo tayari yana wakulima wadogo wadogo wanaoendesha shughuli zao za kilimo, serikali ipange utaratibu wa kuwamilikisha wananchi maeneo husika ili kuondokana na ile dhana ya ’uvamizi’ au kukodishwa ardhi kwa ajili ya kilimo. Zoezi hili lazima lifanywe kwa uwazi ili kuepuka udanganyifu uliotokea katika maeneo mengine ya nchi ambapo vigogo na watu wenye nafasi zao walijitwalia ardhi wakijifanya na wao ni sehemu ya wanakijiji!

Kampuni ya uwindaji yatafuta madini

Kambi hiyo imesema Tanzania imegeuzwa shamba la bibi na kikundi cha mafisadi ambapo imeshuhudia mkataba ilioingiwa baina ya kampuni za Uranium Resourses PLC, Western Metals Limited na Game Frontiers of Tanzania Limited.

Mkataba ambao umetengenezwa na Kampuni ya Kitanzania ya REX ATTORNEYS Machi 23, 2007, unaihusu kampuni ya uwindaji, inayofahamika kwa jina la Game Frontiers of Tanzania Limited inayomilikiwa na Mohsin M. Abdallah na Nargis M. Abdallah.

Mdee alisema kampuni hiyo ya uwindaji, imeingia mkataba na kampuni mbili za kigeni, za kufanya utafiti wa uchimbaji wa madini ya uranium katika Kijiji cha Mbarang’andu.

Alisema sheria za uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka 1974 (Sheria ya zamani) na Sheria mpya The wildlife Conservation Act, Act no 5 of 2009. Sheria hizi zinamruhusu mtu aliye na leseni ya uwindaji, kuwinda wanyama tu.

Aliongeza kuwa kambi hiyo inaitaka serikali ilieleze Bunge uhalali wa mkataba kati ya Game Frontiers na Uranium Resourses PLC na Western Metals.

Mapema akiwasilisha bajeti yake, Waziri wa Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema kuwa wanatarajia kutumia sh bilioni 60 kutoka katika bajeti yao sh bilioni 101.7 ilizoziomba mwaka 2012/2013 kuendeleza mji mpya wa Kigamboni.

Profesa Tibaijuka alisema mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni utahitaji sh trilioni 11.6 mpaka kukamilika kwake na serikali imejipanga kutafuta kiasi hicho cha fedha.

Alisema sh bilioni 60 walizotenga kwa mwaka 2012/2013 ni sawa na asilimia 10 ya fedha zote zinazohitajika katika mradi huo na sh bilioni 605 serikali itatumia mbinu za kisasa kuzitafuta.

Aliziagiza halmashauri za wilaya zote nchini kusimamia ipasavyo masuala ya ardhi kwa kufuata sheria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanaokaidi mipango miji, wanaovamia maeneo ya wazi na kujenga kwenye fukwe hawalipwi fidia.

Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment