Friday 29 June 2012

MADAKTARI 72 WA HOSPITALI YA RUFAA WALIOGOMA WATIMULIWA KAZI -MBEYA


 Mwenyekiti wa Bodi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dk.Norman Sigalla akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu kufukuzwa kazi kwa madaktari hao.
Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari,wakifuatilia taarifa kamili za madaktari waliofukuzwa kazi Mkoani Mbeya.
Mkurugenzi wa wa hospitali ya rufaa Mbeya Dr  E. Sankey akimsikiliza kwa makini kaimu mkuu wa mkoa Mbeya(Picha na Mbeya Yetu)
*******
Habari na Godfrey Kahango,Mbeya.
Sakata la mgomo wa Madaktari  katika hospitali ya Rufaa Mbeya, limeendelea kuingia katika sura mpya baada ya Madaktari 72, waliogoma kutimuliwa na bodi ya hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya.

Hatua ya kutimuliwa  kwa madaktari hao imekuja baada ya bodi hiyo kuwaandikia barua ya kuwataka  kukaa meza moja na kujadili mstakabali mzima wa madai yao ambapo wadaktari hao kukaidi wito huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu Mkuu wa Mkoa  wa Mbeya ambaye pia ni mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dr. Norman Sigalla, alisema kuwa wameamua kusitisha Mkataba wa madaktari hao na kuwarudisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

”Madaktari 54  ni wale walioko kwenye mafunzo ya vitendo kwa mkataba wa miaka miwili  na hospitali ya Rufaa  na madaktari 18 ni wale walioajiriwa na Wizara ya afya” alisema Sigalla na kuwataka wale wote wanaoishi bwenini hospitalini hapo kuwa ifakapo saa 11:00 jioni ya leo(jana) wawe wameondoka katika eneo hilo la hospitali”alisema.

Alisema kuwa wamefikia hatua hiyo kwa kuwa madaktari hao wamekiuka , kuvunja mkataba wawalioingia  na hospitali hiyo pia kukiuka kanuni za kudumu za Umma na toleo la 2009, kifungu namba F16- F. 17 na F27.

 Alisema kuwa madaktari hao waliandikiwa barua ya mara ya kwanza ya kuwaita ili wakutane na Mwenyekiti wa bodi hiyo ya rufaa mbeya lakini walikaidi na kuandikiwa barua ya pili ya kuwataka waeleze kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kutofika kazini kwa siku tano lakini nayo waliikaidi.

Dr. Sigalla akizungumzia kuhusu madaktari  18 ambao ni waajiriwa pia wamo katika mgomo huo alisema kuwa nao wanakabidhiwa barua zao za kusimamishwa ajira zao hospitalini hapo na kuwarudisha Wizarani kwa katibu Mkuu  Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kwa hatua  stahiki za kinidhamu.

“Madaktari waajiriwa wanakabidhiwa barua zao za kusimamishwa ajira yao hospitalini hapa na kuwarudisha Wizarani kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi  wa Jamii kwa hatua stahiki za kinidhamu” alisema Dr. Sigalla.

Hata hivyo gazeti hili lilishuhudia baadhi ya  madaktari hao wakiondoka kwenye mabweni yao huku madaktari hao wakisikika wakisema wapo tayari kurudi walikotoka na kwamba hawapo kuvumilia kile kinachoendelea hivi sasa.

“Tupo tayari kuondoka hospitalini hapa na kurudi tuliko toka wala hatutishiki hata kidogo” walisikika wakisema huku wakiwa wanapakia mabegi yao kwenye tax walizokodi. 

Wakati huohuo Jeshi la Polisi mkoania hapa lilizingira eneo la Hospitali ya Rufaa kuimarisha ulinzi na usalama. 
Source: CHIMBUKO LETU BLOG

No comments:

Post a Comment