Tuesday, 22 May 2012

Wananchi Mali wampiga rais


Wandamanaji wakiwa juu ya kifaru katika ikulu ya Bamako.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeonya kuwa, kitendo cha waandamanaji wenye hasira kumvamia na kumpiga Rais wa muda wa Mali Diancounda Traore hapo jana kinahatarisha mchakato wa kurejesha demokrasia nchini humo.

Ulikuwa kama mchezo wa maigizo pale waandamanaji hao waliojawa na hasira walipovamia Ikulu ya nchi hiyo na kumpa kisago cha mbwa mwitu, rais Traore huku walinzi wake wakitizama.

Hasira za raia hao zilisababishwa na kitendo cha Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magahribi, ECOWAS kumlaazimisha kiongozi wa mapinduzi ya Machi 22 Kapteni Amadou Sanogo akubali kuongeza muda wa serikali ya mpito inyoongozwa na rais Traore kwa miezi kumi na mbili.

Msemaji wa wanajeshi waliyofanya mapinduzi hayo Bakary Mariko, alisema walinzi wa rais Traore waliua watu watatu katika uvamizi huo lakini taarifa nyingine zinasema walinzi hao walikaa na kutizimana huku wananchi hao wakijivinjari katika viwanja vya Ikulu, huku wengine wakiripotiwa kuegesha pikipiki na baiskeli zao katika vyumba vya ikulu hiyo na kuchana picha za rais Traore wakimtaka ajiuzulu mara moja.

Rais ajeruhiwa na kuchaniwa nguo

Katika purukushani hizo rais Traore alichaniwa nguo zake na kujeruhiwa usoni, ambapo alikimbizwa hospitalini kwa matitabu, lakini msaidizi wake alisema rais huyo wa mpito aliruhusiwa kutoka hospitali baadae na kurudi katika makaazi yake binafsi . Haikuafahamika ni lini angerejea Ikulu mjini Bamako.

Mali inakabiliwa na changamoto za mapinduzi ya Machi 22 na uasi kaskazini mwa nchi hiyo. Kapteni Sanogo alikubali mwishoni mwa wiki iliyopita kuacha upinzani dhidi ya kuogezwa kwa muda wa serikali ya mpito, jambo lililowakasirisha wananchi ambao walihamasishwa na wanasiasa wanaounga mkono mapinduzi kuingia mitaani wakimtaka aachie ngazi mara moja.

Waziri Mkuu wa muda Cheick Modibo Diarra alisema kitendo kilichofanywa na wandamanji hao ni cha kusikitisha na kuwataka wanansiasa kuacha kuwahamasisha vijana kufanya vurugu.

Naye balozi wa kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Gerard Araud, ambaye ni moja wa wajumbe wa Baraza la Usalama wanaotembelea kanda ya Afrika Magharibi, alisema vurugu hizo zinazitia mashakani juhudi za Mali kurejesha utulivu , na hali hiyo inaweza kutimiwa vyengine.

ECOWAS yatishia kuchukua hatua

Waziri wa Mambo ya nchi za Nje wa Cote D'voir ambayo ndiyo Mwenyekti wa sasa wa jumuiya ya ECOWAS alilaani kitendo hicho na kusema kuwa Jumuiya hiyo itachukua hatua ambazo zitatangazwa hapo baadae. ECOWAS ilikuwa inatafakari kutuma vikosi vya wanajeshi 3000 kuisaidia Mali kurejesha utulivu upande wa kaskazini lakini maamuzi hayo bado yanajadiliwa.

Waandamanaji hao, ambao walionekana kutokuwa na imani kabisa na wanasiasa nchini humo, walikuwa wakirudia nyimbo za hasira dhidi ya Jumuiya ya ECOWAS ambayo awali ilitishia kumuwekea vikwazo kapteni Sanogo kama asingekubali Rais Traore aendelea kutawala.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\RTRE\AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman

CHANZO DW

No comments:

Post a Comment