Wednesday 11 April 2012

Na Gazeti la mwananchi: Lulu apandishwa kizimbani na kusomewa shitaka lake


Na Mwandishi Wetu

MSANII Elizabeth Michael (Lulu) Leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu na kusomewa mashitaka ya mauwaji yanayomkabili dhidi ya Steven Kanumba.

Elizabeth Michael (Lulu)
Leo hakutakiwa kujibu lolote, kesi imeahirishwa hadi Aprili 24 mwaka huu, amerudishwa rumade kutokana na kesi za mauaji hazina dhamana. Ungana nasi baadaye kwa habari zaidi.


Alichoeleza Lulu polisi hiki hapa

MSANII Elizabeth Michael (Lulu), ameiambia polisi
kuwa kifo cha Steven Kanumba kimetokana na ugonvi kati yao, huku taarifa nyingine zikieleza kuwa huenda Lulu akafikishwa mahakamani leo.

Habari zilizopatikana jana kutoka Kituo cha Polisi Oysterbay zilieleza kuwa, Lulu alisema kuwa kulitokea ugomvi kati yake na Kanumba baada yeye kuzungumza na simu
kutoka kwa mtu maarufu anayetajwa kuwa mpenzi wake.

"Lulu alisema kuwa ugomvi ulitokana na simu aliyopigiwa na mpenzi wake mwingine, ambaye ni mtu maarufu nchini, ndipo
Kanumba akamfokea na ndiyo ugomvi ukaanzia hapo," chanzo hicho kimesema.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa baada ya Kanumba kuanguka, Lulu alitoka nje na kuondoka kwa gari lake hadi maeneo ya Coco Beach, lakini baadaye daktari wa Kanumba alimpigia simu akimtaka arudi ili wampeleke hospitali.

"Alipororudi Sinza ndipo akakamatwa, lakini walikuja Kituo cha Polisi Oysterbay kuchukua PF3," kilisema chanzo hicho.

Chanzo kiliongeza kuwa tangu Lulu alipofikishwa kituoni hapo amekuwa mtulivu asiye na wasiwasi wowote hata katika mahojiano na polisi.

Katika hatua nyingine, Polisi wa kituo hicho jana walipata wakati mgumu baada ya kuibuka kundi la vijana waliotokea makaburi ya Kinondoni kumzika Kanumba, walioandamana wakidai wanamtaka Lulu.
"Tunataka jembe letu", waliimba vijana hao waliofikia 100 wakitokea Barabara ya Ali Hassan Mwinyi huku wakishika majani na kufanya askari waliokuwapo kituoni hapo kuwahi kuchukua silaha na mabomu ya machozi kujiandaa kutuliza ghasia kama zingezuka.

Hata hivyo vijana hao walitawanyika baada ya kuona askari wakiwa tayari kupambana nao na kukimbia maeneo mbalimbali.
Katika hatua nyingine Patricia Kimelemeta anaripoti kuwa,
Msanii Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu huenda akafikishwa mahakamani leo kujibu tuhuma za kuhusika na kifo cha Steven Kanumba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela aliliambia gazeti hili jana kuwa Lulu atafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni mara baada ya polisi kupata ripoti ya vipimo kutoka Mkemea mkuu wa Serikali.

“Tunasubiri ripoti ya Mkemia Mkuu kubaini chanzo cha kifo hicho kwa sababu wamechukua baadhi ya sampuli za marehemu kwenda kupima na kwamba tutakabidhiwa leo(jana). Kimsingi tukipata tu taarifa hiyo tutamfikisha mahakamani,” alisema Kenyela.

Aliongeza ripoti hiyo itaweza kuwasaidia kuandika mashtaka ili yaweze kufikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kumfikisha mahakamani.

Kamanda Kenyela alisema kuwa, ripoti ya madaktari imewasilishwa juzi na kwamba imeonyesha kuwa Kanumba amefariki kwa ugonjwa wa mtikisiko wa ubongo.

Msanii Stephen Kanumba alifariki usiku wa Ijumaa Kuu.

No comments:

Post a Comment