Saturday 25 February 2012

RAIS NELSON MANDELA APELEKWA HOSPITALI

Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, amepelekwa hospitali.
Taarifa rasmi imesema kwamba Bwana Mandela, mwenye umri wa miaka 93, amekuwa na tatizo la tumbo kwa muda mrefu, ambalo linahitaji kushughulikiwa na matabibu.
Kuna ripoti kuwa amepasuliwa.
Msemaji wa rais alieleza kuwa Bwana Mandela ni mzima na amechangamka.
Hii ni mara ya pili kupelekwa hospitali katika mwaka mmoja.
Rais huyo wa zamani aliacha kutokeza hadharani miaka minane iliyopita.
Msemaji wa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Mac Maharaj, alitoa maelezo kuhusu Madiba, jina la jadi la Mandela:
"Tunachotaraji ni ushirikiano wa wananchi na vyombo vya habari, kwamba tuendeshe jambo hili sawasawa.
Tutajaribu kukupeni taarifa.
Sasa ninachoweza kusema ni kwamba, kwa sababu ya faragha yake na familia yake, hatutasema yuko hospitali gani na kadhalika.
Rais Zuma ametuarifu kuwa Rais Mandela alipelekwa hospitali asubuhi.
Kwa muda mrefu Madiba amekuwa akisumbuliwa na tumbo, na madaktari waliamua linahitaji kushughulikiwa na wataalamu.
Tunamuombea afya, na kumhakikishia pendo na nia njema ya wananchi wote wa Afrika Kusini na watu katika sehemu mbali-mbali za dunia."

Source~BBC SWAHILI